Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa kuajiri walimu 4000
wa masomo ya Sayansi na Hisabati. Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam
na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwa katika ziara yake ya kutembela
wilaya mpya za jiji hilo, akianzia na Kigamboni siku ya leo.
Majaliwa amesema mchakato wa ajira hizo unaendelea chini ya
Ofisi ya Rais Utumishi, na muda wowote kutoka sasa mchakato huo
utakapokamilika, majina yatatolewa na walimu hao kuajiriwa.
Kuhusu walimu wa masomo mengine, Waziri Mkuu
amesema walimu wa masomo mengine hususani ya sanaa wapo wa kutosha na
kwamba wanapaswa kusubiri kwakuwa wao wako wengi zaidi na hakuna uhaba na
uhitaji wa walimu hao wa masomo ya sanaa.
Hivi karibuni, Wizara ya Elimu iliwataka wahitimu wa ualimu
katika masomo ya sayansi na hisabati kutuma taarifa (CV) zao ili izihakiki
kabla ya ajira, mchakato ambao tayari umekamilika na majina yalitumwa katika
wizara ya utumishi.
Mhandisi Stella Manyanya - Naibu Waziri wa Elimu
Kituo
kimoja cha redio nchini kilizungumza na Naibu Waziri wa Elimu, Mhandisi Stella
Manyanya wiki mbili zilizopita ambapo alisema kuwa kazi ya wizara yake ilikuwa
ni kuhakiki taarifa za wahitimu hao, na si kuajiri, huku akibainisha kuwa zoezi
hilo limekamilika na majina yako utumishi ambao ndiyo watahusika na kuajiri.
Pia alisisitiza kuwa kama wizara ya elimu waliomba kupewa
walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati haraka kwa kuwa uhitaji wao ni mkubwa
zaidi na kuwataka wahitimu wote waliotuma taarifa zao, wasubiri watapata majibu
muda si mrefu.
Katika hatua nyingine Majaliwa amewaagiza wakurugenzi
wa halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam kufuta malipo ya posho zote za vikao
visivyo rasmi (vikao vinavyoibuka bila sababu maalum) pamoja na fedha za
vitafunwa na fedha hizo zipelekwe kwenye miradi ya maendeleo na ametaka
zoezi hilo lianze mwezi huu wa Januari 2017.
Pia ametoa siku 3 kwa watumishi 10 waliohamishwa kutoka
Wilaya ya Temeke kuhamia Wilaya ya Kigamboni wawe wameripoti katika Wilaya hiyo
ya Kigamboni vinginevyo ameelekeza mamlaka husika kuwafuta kazi na wasiwe tena
kwenye ajira ya serikali.
No comments:
Post a Comment