Picha kwa msaada wa google
Katika Makala iliyopita tuliangalia mambo muhimu ya kuzingiatia au vipengele muhimu katika wasifu wa kazi.
Wasifu wa kazi ni nyaraka muhimu sana.Umuhimu wake siyo tu kwa watafuta ajira lakini hata wale wenye ajira tayari. Wasifu wa kazi husaidia kuonesha uwezo na ubora wako wa kitaaluma na katika utendaji wa kazi. Wasifu pia ni nyaraka inayoweza kukusaidia kuuza ujuzi wako kwa watu na mashirika ambayo yanaweza kuhitaji kukuajiri au kukutumia katika shughuli fulani.
Wasifu wa kazi ni nyaraka muhimu sana.Umuhimu wake siyo tu kwa watafuta ajira lakini hata wale wenye ajira tayari. Wasifu wa kazi husaidia kuonesha uwezo na ubora wako wa kitaaluma na katika utendaji wa kazi. Wasifu pia ni nyaraka inayoweza kukusaidia kuuza ujuzi wako kwa watu na mashirika ambayo yanaweza kuhitaji kukuajiri au kukutumia katika shughuli fulani.
Umuhimu wa wasifu wa kazi unaonesha dhahiri ni kitu kinachatakiwa kiandaliwe kwa ustadi na umakini mkubwa. Pamoja na ukweli huu bado kuna makosa ya mara kwa mara yamekuwa yakifanywa na waandishi wengi wa wasifu yanayofanya nyaraka hii muhimu kukosa ushawishi na pengine kupuuzwa na waajira hasa kwa wale wanaotafuta ajira.
Je ni makossa yapi yanaweza kufanya wasifu wako usionekane bora?
MAKOSA YA KIUANDISHI
Kutokana na kukosa umakini au kutojiridhisha baada ya kuandaa wasifu makosa mengi ya kiuandishi huonekana kwenye nyaraka hii. Ifahamike kuwa kukosea ni kitu cha kawaida katika uandishi wakati mwingine kwa kujua au kutokujua. Unapoandaa wasifu wako ni vyema kupitia mara kadhaa na kujiridhisha kama hakuna makosa yoyote ya kiuandishi. Inashauriwa pia kumpa mtu mwingine akusaidia kupitia kama kuna makosa mengine yoyote unayoweza kuwa umeyaacha. Ifahamike kuwa waajiri wanaweza kuachana kukuita kwenye usaili kwa sababu tu wasifu wako na makosa ya kiuandishi.
UANDISHI USIOWIANA
Wasifu wako unatakiwa kuwa na mtindo na ukubwa wa maandishi unaowiana. Wasifu unapochapwa kwa kompyuta unaweza kuandika kwa kutumia mitindo mbali mbali kama Times New Romans na mingine. Hakikisha unatumia mtindo mmoja kwa wasifu wote huku ukubwa wa maandishi pia ukiwa sawa japo unaweza tofautisha kwa kuonesha tofauti ya maandishi katika vipengele au vichwa kama neno ‘Ujuzi”. Ikumbukwe kuwa vichwa vyote vinatakiwa kuwa sawa pia. Hakikisha hutumii rangi nyingi katika wasifu wako. Rangi nyeusi pekee inafaa kwa kuandika wasifu wako wote.
KUWEKA VIPENGELE AU MAMBO YASIYO NA UMUHIMU
Siyo kila kitu ni cha kuandika au kuweka kwenye wasifu wako wa kazi. Unapotaka kuweka au kuongeza kitu kwenye wasifu wako wa kazi jiulize kama kinauhusiano na hiyo kazi au kinaweza kukuuza vipi kwa mwajiri. Baadhi ya mambo yanapoandikwa au kuwekwa kwenye wasifu yanaweza sababisha ukabaguliwa au kuonekana haufai kwa kazi husika. Mambo kama imani yako ya dini si muhimu kwani hayana msaada wowote kwenye kushawishi kuajiriwa kwako na yanaweza sababisha ukabaguliwa kama anayepitia wasifu atakuwa wa imani tofauti au inayokinzana na yako. Kama unaomba ajira kwenye shirika la dini na unahisi kutaja dini yako kutakuongezea nafasi ya kuchaguliwa au kuajiriwa si vibaya kuainisha imani yako.
Endapo unaomba ajira na mwajiri hajaainisha kuwa uweke picha yako pia si vyema kuambatanisha kwenye wasifu wako kwani inaweza kuwa chanzo cha kubaguliwa kwa sababu mbali mbali. Je, unahisi wewe una sura nzuri sana hivyo itashawishi kuajiriwa kwako? Kama jibu ni ndiyo, inaweza isikusaidie na ikakuletea madhara. Yupo mtu anaweza akajisemea tu, “huyu mdada alivyo mzuri tukimchagua atakuja kuongeza ushindani na kutuchukulia mabwana zetu hapa”. Usishangae, duniani kuna vituko.
MATUMIZI YA WASIFU MMOJA KWA KILA HITAJI.
Hata kama umeuandika wasifu wako kwa ustadi wa hali ya juu kumbuka kwamba hauwezi utumia huo wasifu kwa matumizi yote. Kama unaomba kazi ya uhasibu wasifu utakao utumia hautakiwi kuwa sawa na ule utakao utumia ukiwa unaomba kazi ya Afisa wa benki. Kila kazi ina mahitaji yake hivyo unatakiwa uhakikishe kuwa wasifu wako unakidhi mahitaji ya kazi husika. Katika Makala yaliyopita tuliona kuwa kuna kipengele muhimu cha Ujuzi katika wasifu, ujuzi wa kazi moja mara nyingi siyo ujuzi wa kazi nyingine hivyo ni muhimu kuzingatia mahitaji ya kazi husika.
UREFU WA WASIFU
Watu wengi hudhani kuwa kuwa na wasifu wenye kurasa nyingi kuna kupa nafasi ya kuonekana wewe ni bora kuliko yule mwenye wasifu wenye kurasa chache lakini kinyume chake kinaweza kuwa sawa kwa baadhi ya mazingira. Waweza andaa wasifu wa kurasa kumi lakini mwenye wasifu wenye kurasa mbili tu akaonekana ni bora zaidi kuliko wewe. Ni vyema kuzingatia vitu vya msingi vya kuweka kwenye wasifu wako na kuviweka katika mpangilio mzuri. Haina haja ya kuonesha alama ulizopata kwa kila somo ulipokuwa chuoni. Kama mwajiri atahitaji hili ambatanisha matokeo yako (transcript).
Hakuna mtu mwenye muda wa kupitia kurasa nyingi za wasifu wako wenye vitu visivo vya msingi. Ikumbukwe pia kwa baadhi ya kazi kama uhadhiri wasifu utahitaji kuonesha idadi ya machapisho ya kitaaluma aliyoyachapisha muhusika bila kujali idadi hivyo ni urefu wa wasifu katika mazingira haya unaweza usiwe shida.
UTOAJI WA TAARIFA ZISIZO ZA KWELI
Ili kuwashawishi waajiri wapo watu wanaoamua kutoa taarifa zisizo za kweli kwa lengo la kuwahadaha waajiri. Moja ya vipengele vinavyoongoza katika kuweka taarifa zisizo za kweli ni kile cha uzoefu. Kwa namna teknolojia ilivyokua ni rahisi kwa mtu kujiridhisha kama ni kweli taarifa ulizo zitoa ni za kweli au ni vinginevyo. Kusema kwamba ulishawahi kufanya kazi na shirika fulani wakati siyo kweli kunaweza kukufanya uonekane si mwaminifu na hivyo kuaharibu sifa yako. Wadhamini uliowaweka wanawezakupigiwa simu kujiridhisha lakini pia hata hilo shirika uliloliainisha kwenye wasifu wako laweza kupigiwa simu.
MATUMIZI YA BARUA PEPE ZISIZO ZA KIWELEDI
Barua pepe yako inabidi ioneshe namna gani uko makini na unachokifanya. Kama unaitwa Mabuga Salamba kuwa na barua pepe kama msalamba@yahoo.comau mabugasalamba@gmail.com au yoyote inayoonesha majina yako bila mbwembwe zozote inashauriwa. Epuka matumizi ya baruapepe kama dopeboy@yahoo.com, sweetmangi@gmail.com au zinazofanana na hizi. Zitaonesha kuwe wewe ni mtu ambaye haupo makini na pengine una utoto.
(Makala haya yalichapishwa kwenye gazeti la Nipashe tarehe 18 Novemba, 2017)
No comments:
Post a Comment