KUNA mfumko mkubwa
wa kilimo cha bangi nchini; na sasa baadhi ya watu wanaendesha kilimo cha dawa
hizo za kulevya kwa kutumia teknolojia ya umwagiliaji.
Wengine wanalima
bangi katikati ya hifadhi za misitu ya taifa na juu ya milima, ambako ni vigumu
kwa usafiri wa gari au pikipiki.
Wakati kilimo cha
bangi kinashamiri, pia kumekuwepo na ongezeko la watuhumiwa waliokamatwa kwa
tuhuma za kujihusisha na dawa zingine za kulevya kama mirungi, kokeni na
heroin. Ongezeko hilo linatokana na kazi inayofanywa na kikosi kazi,
kinachoundwa na taasisi mbalimbali kuzidisha msako.
Kikosi kazi hicho
kinaundwa na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Polisi, Uhamiaji, Mamlaka ya
Mapato, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Jeshi la Wananchi, Magereza na Takukuru.
Kikosi kazi hicho
kinapambana na watuhumiwa wanaojihusisha na uingizaji, usambazaji na utumiaji
wa dawa za kulevya.
Akizungumza na
gazeti hili jana, Kamanda wa Kikosi cha Dawa za Kulevya nchini, Mihayo Msikhela
alisema mwaka huu zimekamatwa kilo 84.183.6 za dawa za kulevya, ukilinganisha
na kilo 35,373 zilizokamatwa mwaka jana. Idadi ya watuhumiwa pia imeongezeka
kutoka 14,339 mwaka jana hadi kufikia watuhumiwa 18,893 waliokamatwa mwaka huu.
Kilimo cha bangi
Akizungumzia kilimo cha bangi, Msikhela alisema kikosi kazi hicho, kimebaini
kulimwa zao hilo kwa wingi katika safu za milima mbalimbali nchini, ambako
kutokana na jiografia ya huko ni vigumu kufika kwa usafiri wa gari au pikipiki.
“Bangi ni janga la
taifa, watu wamegeukia kilimo cha bangi na kuacha kulima mazao mengine katika
maeneo mengi nchini. Walimaji wanalima katika maeneo ambako ni ngumu kuyafikia
kwa usafiri wa magari au pikipiki,” alisema Msikhela.
Alisema kutokana na
msako mkali wa kikosi kazi hiyo, mwaka huu kumekuwa na kesi nyingi na kiasi
kikubwa cha bangi iliyokamatwa ukilinganishwa na mwaka jana.
Alisema mwaka huu
kumekuwa na kesi 8,159 zilizohusu bangi wakati mwaka jana kulikuwa na kesi
6,752. Ongezeko la kesi za bangi ni 1,407. Kiasi cha bangi ambacho kimekamawa
mwaka huu ni kilo 65,804, tofauti na mwaka jana ambako bangi iliyokamatwa
ilikuwa ni kilo 20,066.
Idadi ya watuhumiwa
wa bangi, pia imeongezeka kutoka watuhumiwa 12,056 hadi kufikia watuhumiwa
15,800. Alisema wamebaini kuwepo kwa kilimo cha umwagiliaji wa zao la bangi
katika bonde la mto Ruvu kuelekea wilaya za Kisarawe na Morogoro.
“Bonde lote lile
watu wanalima bangi kwa kutumia teknolojia ya umwagiliaji, juzi tu tumegundua
kuwepo kwa hekta 30 za mashamba ya bangi kwenye bonde hilo na tukaziteketeza,”
alisema.
Pia alisema kikosi
kazi hicho, wamebaini kuwepo kwa mashamba mengi ya bangi katika safu za milima
ya Udzungwa. Alifafanua kuwa katika maeneo hayo, wakulima wanaenda milimani
ambako ni ngumu kufika na huko wanapanda bangi.
“Hivi juzi Polisi
tuliendesha operesheni maalumu ya kutokomeza bangi katika baadhi ya maeneo
ikiwemo katika milima ya Kikewe na Mgeta, ambapo tulishuhudia bangi hiyo ikiwa
imestawi katika ekari 20 za mashamba yaliyoko milimani,” alisema Musikhela.
Anasema licha ya
kuteketeza mashamba hayo, lakini walikamata magunia 200 yakiwa yamehifadhiwa
kwenye nyumba ambazo zimejengwa maalumu huko milimani kwa ajili ya kuhifadhi
bangi. Alitaja kilimo cha bangi ambako kimeshamiri kuwa ni Morogoro, Tarime,
Arusha, Iringa, Ruvuma na Simiyu.
“Mikoa hii inaongoza
kwa kilimo cha bangi na tumekuwa tunafanya kazi nzito ya kusaka mashamba kwa
kuwashirikisha wananchi. Dawa zingine za kulevya Akizungumzia mapambano dhidi
ya dawa zingine za kulevya, Msikhela alisema kazi inayofanywa na kikosi kazi
imesaidia kupungua kwa dawa za viwandani, zinazoingizwa nchini kutoka Asia na
Amerika."
Alitoa mfano kuwa
mwaka huu, wamekamatwa watu 250 walioijngiza cocaine nchini, tofauti na mwaka
jana walikamatwa watuhumiwa 258. Hata hivyo, alisema kikosi hicho kimekamatwa
kilo 18 za dawa hizo, tofauti na mwaka jana walikamata kilo 8.
Lakini, idadi ya
kesi pia imeongezeka kutoka kesi 107 hadi kufikia kesi 181 na hivyo kuwepo
ongezeko la kesi 74.
Kwa upande wa
heroin, idadi ya kesi imeongezeka kutoka 289 hadi kufikia kesi 415 ongezeko
likiwa ni kesi 126, idadi ya watuhumiwa waliokamatwa imeongezeka kutoka
watuhumiwa 482 hadi kufikia 640 na kilo zilizokamatwa, zimeshuka kutoka kilo
69.3 hadi kufikia kilo 31.7.
Kwa upande wa
mirungi, idadi ya kesi imeongezeka kutoka 1,071 hadi kufikia 8,159, hivyo
kufanya kuwepo kwa ongezeko la kesi 233, idadi ya watuhumiwa imeongezeka kutoka
1,543 hadi kufikia 2,203 na kiasi cha dawa kilichokamatwa kimeongezeka kutoka
kilo 15,229.6 hadi kilo 18,329.8 mwaka huu.
Alisema changamoto
kubwa wanayokabiliana nayo ni mipaka ya Bahari ya Hindi kuwa mrefu, jambo
ambalo linafanya kuwepo ugumu wa udhibiti wa uingizaji wa dawa za kulevya. Pia
alisema kwa sasa watuhumiwa wengi, wanatumia Mto Ruvuma mpakani na Msumbiji,
kuingiza dawa za kulevya kutokana mpaka huo pia kuwa mrefu.
No comments:
Post a Comment