Friday, 9 December 2016
Makala ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika na balozi Liundi
Judith Mhina – MAELEZO
SERA YA VIWANDA ITATUKOMBOA
Katika kuadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika Idara ya Habari – MAELEZO ilipata fursa ya kufanya mahojiano na Mwanasiasa na mwana Diplomasia Balozi Christopher Liundi kuhusiana na maadhimisho hayo. Yafuatayo ni maswali na majibu katika mahojiano hayo:
SWALI: Mheshimiwa Balozi Tanzania imetimiza miaka 55 ya Uhuru una lipi la kuwaeleza Watanzania?
JIBU: Kwa mtazamo wangu nina mambo matatu muhimu ninayoayaona katika hii miaka 55 ya Uhuru. Jambo la kwanza lazima tutambue na tuone fahari kwa nchi yetu kufikisha miaka 55, bila kuwepo na machafuko yalliyosababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Katika miaka 55 tumeweza kujitawala kwa amani na utulivu kutokana na viongozi wetu kuwa na busara na kutongangania madaraka kama ilivyo kwa nchi nyingine barani Afrika.
Pili, tumeweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo katika nyanja mbalimbali kama vile elimu, afya, miundombinu , uchukuzi na viwanda. Katika elimu kwa mfano wakati wa ukoloni kulikuwa na shule za Wazungu, Wahindi na Waafrika lakini sasa, watoto wote wanasoma bila kujali kama ni Mzungu Mhindi au Mwafrika.
Mwisho, nakumbuka mara baada ya Uhuru tukaja na sheria zetu, baraza letu la mawaziri na maamuzi yetu wenyewe. Misingi hiyo tumeidumisha na kuridhisha kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo Yapo mambo mengi ambayo tunaweza kukumbuka ambayo hayakuwa mazuri lakini la muhimu ni lazima ukisema uhuru umkumbuke Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage. Nyerere ambaye alitumia muda wake wote, uwezo wake wote pamoja na waasisi wa TANU kuhakikisha nchi hii inakuwa huru.
SWALI: Mheshimiwa Balozi wewe ni kati ya watu waliobobea katika siasa na Diplomasia za nchi na umefanya kazi na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Unadhani muelekeo tulionao mpaka sasa unaleta hali halisi ya nchi huru katika miaka 55 ya Uhuru?
JIBU: Muelekeo ni mzuri tena madhubuti. Umeleta matumaini makubwa mno kutokana na kuweza kuendelea na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lakini pia huduma zinazotolewa na serikali yetu kwa wananchi kukua, kuimarika na kuboreshwa zaidi.
Pili kuna hali ya amani inayowafanya watu washiriki katika kujenga uchumi na kujiletea maendeleo. Mfano kuweka miundombinu ili kukuza uchumi ambapo barabara zimejengwa nchi nzima kwa kuunganisha Mikoa na Mkioa, Wilaya na Wilaya na sasa tunaelekea kuunganisha Tarafa Kata na hatimaye vijiji. Hii ni dalili nzuri ya maendeleo na kukua kwa uchumi.
Tatu , kuongezeka kwa wataalam wetu wenyewe katika taaluma mbalimbali ambapo wakati tunapata uhuru tulikuwa na wataalamu wachache sana, sina takwimu lakini sasa Mtanzania anaweza kuongoza meli, ndege, kuchimba madini na kutengeneza barabara. Nani alitegemea Mtanzania atatengeneza barabara hapa nchini? Nani alidhani mtanzania anaweza kurusha ndege? Nani alidhani Mtanzania naweza kuchora mchoro wa majengo marefu tuliyonayo hivi leo.
Haya yote yanaonyesha kwamba muelekeo wetu unaleta matumaini na uko sahihi. Tumpe Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Tano ushirikiano ili aweze kutimiza ndoto zetu.
SWALI: NIni maoni yako kuhusu nchi muelekeo wa nchi kwenye uchumi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa?
JIBU: Tukubali kuwa uchumi ndio msingi wa maendeleo wa Taifa lolote. Sera zinazoandaliwa ni lazima zilenge katika kuleta maendeleo ya nchi kiuchumi. Rais anaposema anataka Taifa liondokane na umasikinini ni kweli tutaondokana nao, kama tutakuwa na viwanda vidogo vya kati na vikubwa. Kutokana na viwanda watu watapata ajira Wakulima watapata sokola uhakika la mazao yao na bidhaa zitakazozalishwa zitauzwa ndani na nje ya nchi kwa kuwa zimeongezewa dhamani.
Watanzania tumekuwa na tatizo la kuthamini vitu vinavyotoka nje. Mfano mzuri ni China ambao viwanda vyao vilianza kuzalisha bidhaa ambazo zilitumika nchini mwao hadi kujitosheleza. Hivi sasa nchi hiyo imepata soko kubwa la nje na uchumi wake umeendelea kukua.
SWALI : Suala la nidhamu kwa Watumishi wa Umma, Taasisi, Mashirika na Idara za Serikali mara baada ya Uhuru na sasa miaka 55 ya Uhuru?
JIBU: Nidhamu ni suala la msingi mahali popote na sio mahali pa kazi tu hata nyumbani kwako. Watanzania walizoea kufanya kazi kwa mazoea na hivyo kukosa nidhamu. Utendaji kazi mzuri unatokana na nidhamu ambayo inamfanya mtu afanye kazi kwa uadilifu.
Nidhamu katika Utumishi wa Umma inayosisistizwa na Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli Itaongeza bidii ya kazi kwa wafanyakazi viwandani na hivyo kuongeza uzalishaji. Enzi za Baba wa Taifa Wafanyakazi na Wakulima wote walikuwa na nidhamu na uwajibikaji ulikuwa mkubwa zaidi ndi maana uchumi wa nchi ulikuwa wa juu. Kila mtu aliwajibika mahali pake pa kazi.
Enzi za Baba wa Taifa unapokwenda popote duniani, ukisema niketoka Tanzania kila mtu anajua Mtanzania ni mkweli, muwazi na ana nidhamu ya hali ya juu. Mtanzania hawezi kupokea wala kutoa rushwa, hashiriki kwenye masuala yoyote ya kuiharibia heshima nchi yake, mwenye kutumia madaraka yake vizuri, na asiyefuja mali ya umma.
SWALI:: Msaada gani unaweza kumpa Mhe Rais katika vita dhidi ya wakwepaji kulipa Ushuru?
JIBU: Kwanza namshukuru sana Rais katika suala zima la ukusanyaji kodi kwani ameonyesha umuhimu kwa kulipa kodi
Pili, nampongeza kwa kuanzisha mfumo unaomtaka kila mfanyabiashara kuwa na mashine za kulipa kodi. “Mpaka sasa imefikia mahali nchi nyingine za nje wameanza kuiga utendaji wa kazi wa Rais wetu hili ni jambo la kujivunia”. Hivyo tumuunge mkono katika hii vita ya ukusanyaji kodi. Watanzania wakubali mpaka sasa kwamba hatua alizochukua Mheshimiwa Rais za kukusanya kodi ni sahihi na tuziunge mkono.
Tatu, Serikali haina namna itakayoweza kupata fedha za kusaidia watu wake kupata huduma za msingi. Fedha zinazokusanywa ndio zinazotumika kwenye barabara, kununulia madawa kujenga Hospital na mabo kama hayo.
SWALI :Unaposikia siku ya Uhuru wa Tanganyika unakumbuka nini?
JIBU: Hii inanikumbusha kauli ya Mwalimu Nyerere alisema: “UHURU NA KAZI”, ni kweli kabisa lazima tufanye kazi kama anavyosisitiza Rais wetu Magufuli “HAPA KAZI TU”. Maendeleo hayaji kwa kupiga hadithi ni lazima watu wafanye kazi na asiyefanya kazi na asile.
Pili siku hii ya Uhuru inanikumbusha juu ya elimu ambayo wakati huo inatolewa bure, lakini baadaye ilisitishwa na kuwafanya vijana wengi kukosa fursa ya kuendelea na masomo . Rais wetu ameamua elimu sasa itolewe bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari ili kuwaondolea mizigo wazazi ambao walishindwa kuwasomesha watoto wao kutokana na gharama kubwa.
SWALI: Una wito gani kwa Watanzania katika kusheherekea miaka 55 ya Uhuru?
JIBU: Wito wangu kwa Watanzania tusikilize maelekezo yanayotolewa na serikali yetu ambayo ni sikivu, tuisipende kusikiliza maneno ambayo sio rasmi na kujiamulia jambo bila kufuata sheria.Watanzania tufanye kazi tuache uvivu tusipende kulaumu serikali wakati sisi wenyewe tunakaa tu bila kufanya kazi. Tuunge mkono Serikali yetu kwa kila jambo inayoelekeza kufanya.
Waandishi wa Habari wanafanya kazi nzuri sana ya kuelimisha. Napenda kuwapongeza kwa hilo. Waaendelee kuelimisha jamii kwa kuelezea masuala ya msingi na muhimu katika maendeleo yao na hasa nchi kwa ujumla.
Mwisho tuendelee kulinda Muungano wetu Amani yetu, Upendo, Umoja na Mshikamano.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment