HATUA ya Shirika la Umeme ya
kupandisha bei ya umeme bila kushirikisha mamlaka nyingine za Serikali,
zimemgharimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Felchesmi Mramba, ambaye jana
amefutwa kazi na Rais John Magufuli.
Kabla ya kutengua uteuzi wa Mramba,
Rais Magufuli ambaye jana alisali mjini Bukoba katika kanisa la Bikira Maria,
Mama mwenye Huruma la mjini Bukoba, alisema Tanesco haikumshirikisha yeye,
Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Ewura juzi ilitangaza kupandisha bei
ya umeme kwa asilimia 8.5 baada ya Tanesco kuomba gharama zipande kwa asilimia
18.19, lakini hatua hiyo ilisitishwa na Profesa Muhongo.
“Waliopandisha umeme hawakuja
kuniuliza hata mimi kiongozi wa nchi, hawakuuliza hata waziri mwenye dhamana,
ya nishati hawakumuuliza hata Makamu wa Rais, Waziri Mkuu haiwezekani mtu akae
pekee yake na afanye maamuzi yake pekee bila kushirikisha mamlaka nyingine,”
alisema Rais.
Ateua bosi mpya
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU, Gerson Msigwa ilieleza kuwa Rais Magufuli baada ya
kutengua uteuzi wa Mramba, amemteua Dk Tito Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa Tanesco.
Mwinuka ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam(UDSM) na hadi uteuzi wa jana, alikuwa ni Mkuu wa Idara ya
Mekanika na Uhandisi wa Viwanda Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) cha Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.
Akiwa kanisani, Rais Magufuli
alimpongeza Profesa Muhongo kwa hatua ya kusimamisha kupanda kwa bei ya umeme.
“Namshukuru waziri wa nishati kwamba
ameshatengua maamuzi hayo, kwa hiyo umeme hakuna kupanda.” Rais Magufuli
alisema haiwezekani watu mnapanga mikakati ya kujenga viwanda na hasa katika
mikakati hii mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme hadi vijijini na umeme huo
unaenda hadi kwa watu maskini walioumbwa kwa mfano wa Mungu, halafu mtu pekee
kwa sababu ya cheo chake anakwenda kusimama kupandisha bei ya umeme.
Akionekana kukereka kwa hatua hiyo ya
kupandishwa kwa bei ya umeme, Rais Magufuli alisema, “Na ndio maana baba askofu
nalizungumza hili kwamba majipu bado yapo na nitaendelea kuyatumbua, ndio maana
naomba sana Watanzania muendelee kutuombea, lengo la serikali ninayoiongoza ni
kwenda na wananchi wa kipato cha chini.”
Prof Muhongo alivyoikaanga Tanesco
Juzi usiku
Profesa Muhongo alimwandikia barua
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi
ya kumtaka kusitisha ongezeko la bei ya umeme iliyokuwa ianze kutumika jana.
Profesa Muhongo alitoa uamuzi huo chini ya sheria ya umeme ya mwaka 2008 ambayo
inampa mamlaka waziri mwenye dhamana ya nishati.
“Leo Desemba 31, 3016 Ewura
inaamuliwa kusitisha utekelezaji wa bei mpya za umeme uliyotangaza jana hadi
hapo Serikali itakapopitia ripoti ya Ewura.”
Akizungumza na kituo kimoja cha radio
jana, Profesa Muhongo alisema alisitisha uamuzi wa Ewura kwa sababu taratibu
hazijafuatwa. Alisema pia Watanzania wote waliohojiwa walipinga ombi la Tanesco
la kupandisha umeme.
“Ewura walitumia kigezo gani cha
kuongeza bei, kama walitumia kigezo ambacho wengi hatukijui basi huo ni uamuzi
wao wenyewe,” alisema.
Alisema taratibu zilizopo ni kwamba
mara Tanesco wanapoomba kupandisha bei za umeme na Ewura ikishasikiliza maoni
ya wadau, kabla ya kutangaza uamuzi ni lazima waziri mwenye dhamana na nishati
ajulishwe kwanza.
“Lakini hivi ninavyozungumza na wewe
hata mimi nilishtushwa jana naambiwa Ewura wametangaza, mimi nilikuwa sijapata
chochote kutoka Ewura, mimi sijajadiliana na Ewura wala sijajadiliana na
Tanesco kutokana na zoezi zima la kutaka kuongeza bei,” alisema.
Alisema waziri hashirikishwi ila
anatakiwa kupokea taarifa ya mwisho, “hadi leo nimesikia tu, sijapokea hiyo
taarifa, nenda kawaulize Ewura na Tanesco kama nina ripoti yao ya mwisho.
Alisema matatizo ya Tanesco
hayatatuliwi kwa kuongeza bei, alisema matatizo ya shirika yanatokana na
uongozi wa Tanesco na mambo mengine ambayo yanafahamika.
Alisema Ewura lazima ipeleke
mapendekezo yake Wizara ya Nishati na Madini. Profesa Muhongo alisema hapo
ndipo waziri atawaita Ewura na Tanesco kujadiliana na wakikubaliana hapo ndipo
wataenda kutangaza hiyo bei.
Alisema haiwezekani Ewura ni chombo
cha Serikali hivyo haiwezi kufanya bila waziri kufahamu.
Alisema tatizo la madeni ya Tanesco
sio kuongeza bei ya umeme, alisema Serikali kwa sasa imefuta fedha za mikopo ya
nje kwa ajili ya kulipa deni la Tanesco, hatuwezi kutafuta fedha za kulipa deni
za kulipa madeni hayo kwa Watanzania halafu shukrani iwe ni kuongezewa bei ya
umeme.”
Alisisitiza kuwa matumizi ya fedha ya
Tanesco ni mabaya kwa sababu kila mwisho wa mwaka viongozi peke yake wanalipana
bonus na akatoa mfano wa mwaka jana alifuta maamuzi hayo wakati tayari viongozi
wameshapitisha uamuzi wa kulipana kati ya Sh milioni 60 na Sh milioni 40.
“Hivi kweli Tanesco wanafanya kazi
nzuri, wanatuongezea bei ili walipane posho?” aliuliza.
Ahadi ya wizara kwa umma Waziri
Muhongo akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka
2016/17 ya wizara hiyo bungeni mjini Dodoma mwaka jana kuhusu upatikanaji wa
huduma ya umeme nchini, alisema kiwango cha upatikanaji wa huduma ya umeme
(access level), kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Watanzania waliofikiwa na huduma
hiyo, ameongezeka kutoka asilimia 36 mwezi Machi 2015 hadi kufikia takriban
asilimia 40 mwezi Aprili, 2016.
Alisema ongezeko hilo limetokana na
juhudi za Serikali za kusambaza umeme nchini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Kuhusu punguzo la viwango vya bei za
umeme, Profesa Muhongo alisema Serikali imetekeleza ahadi yake ya kupunguza bei
za umeme kuanzia Aprili Mosi mwaka 2016 kwa kati ya asilimia 1.5 na 2.4.
Alisema Serikali pia imeondoa tozo ya
kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa umeme (application fees) ya Sh 5,000 na
tozo ya huduma ya mwezi (service charge) ya Sh 5,520 kwa Wateja wa Umeme kwa
Daraja la T1 na D1, ambao wengi wao ni wa majumbani.
Hatua hii itawasaidia watumiaji
wadogo wa umeme mijini na vijijini kumudu gharama hizo, hivyo kuboresha
shughuli za kijamii na kiuchumi Ewura ilivyobariki ongezeko Juzi Ewura
ilitangaza kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 badala ya asilimia 18.19
iliyokuwa imeombwa na Shirika la Umeme Nchini (Tanesco).
Bei hizo mpya ilikuwa zianze kutumika
jana Januari mosi, 2017. Akitangaza ongezeko hilo la bei, Mkurugenzi Mkuu wa
Ewura alisema, mamlaka yake imefikia uamuzi wa kuongeza asilimia 8.5 kutokana
na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wake.
Shirika la umeme Zanzibar (ZECO)
ambalo linanunua umeme wa jumla kupeleka Zanzibar limeongezewa kwa asilimia 5.7
ya bei ya umeme.
Ongezeko hilo halikuwahusu wateja wa
majumbani ambao matumizi yao hayazidi uniti 75 kwa mwezi ambao wengi ni
wananchi wa vijijini ambao wanatumia umeme kwa kuwasha taa tu.
Sababu kupandisha umeme
Oktoba mwaka huu Tanesco iliomba
kupandisha bei za umeme kwa maelezo kuwa gharama za uendeshaji katika
uzalishaji na usafirishaji wa umeme zilikuwa juu hivyo kuna haja ya kupandisha
bei za umeme.
Hatua hiyo ilikuja ikiwa ni miezi
saba tangu kutangazwa kwa bei mpya ya umeme iliyokuwa na punguzo la asilimia
1.5 hadi 2.4 sanjari na kuondoa tozo ya kuunganishiwa umeme ya Sh 5,000 na
gharama ya huduma kwa kila mwezi ambayo ilikuwa na Sh 5,520.
Wakati inaomba kupandisha bei
aliyekuwa mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema ombi la mabadiliko ya
bei za umeme ambalo waliliwasilisha Ewura Oktoba mwaka jana ni kutokana na
agizo la kubadilisha bei za umeme la mwaka 2016 lililoanza kutumika Aprili 2016.
Alisema ifahamike kuwa bei za umeme
zilitolewa zilitakiwa zitumike mpaka 31/12/2016, hivyo itakapofika Januari 2017
inatakiwa bei mpya za umeme kutolewa kwa mujibu wa sheria.
“Hivyo Taneso ilitakiwa kufanya
tathmini ya gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme na kupeleka
mapendekezo hayo kwenye Ewura ili kupitiwa na kufanyiwa taftishi, kupata maoni
ya wadau ikiwa ni pamoja na baraza la ushauri la Serikali."
Hivyo basi ikiwa bei za umeme
zitapanda au kutopanda, hiyo itategemea na mapitio ya tathmini ya gharama za
kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme tulizowasilisha Ewura.
Alisema Tanesco haiwezi kuamua
yenyewe kupandisha au kutopandisha bei za umeme.
Aliongeza kuwa kupanda au kushuka kwa
gharama za umeme ni suala la kisheria na ni jambo la kawaida kwani bei ya umeme
imeshawahi kushuka katika vipindi tofauti.
Mramba alitoa mfano mwaka 2015 robo
ya kwanza ya mwaka bei ilishuka kwa asilimia 2.5 na vivyo hivyo Aprili mwaka
2016 pia gharama za umeme zilishuka kwa asilimia 1.6.
Askofu Kilaini asifia Katika mahubiri
yaliyoendeshwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius
Kilaini, alipongeza jitihada za Rais Magufuli hasa kuhakikisha analeta usawa na
uwajibikaji kwa watendaji wa Serikali.
Askofu Kilaini alisema hali ya sasa
kwa utendaji wa Serikali imebadilika kwani huko katika ofisi zaumma hakuna
usumbufu wa kusubiria mtumishi, wala hakuna ile tabia ya kuombwa kitu kidogo
“Ile kauli ya unatuachaje kama ilivyokuwa imezoeleka kwa baadhi ya watumishi
katika sekta za umma sasa haipo tena.”
Kilaini aliwataka Watanzania kutumia
sherehe za mwaka mpya 2017 kujitathmini na kuondoa changamoto mbalimbali
zilizojitokeza hasa kwa mwaka uliomalizika 2016, hususani kama majanga ya
tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10 mwaka jana na kusababisha maafa
makubwa mjini Bukoba.
“Tetemeko lililotokea Kagera sio
nyundo ya kuwahimiza,bali ni kengele ya kutufanya tusonge
mbele!hivyo,Watanzania tujielekeze kujituma kufanya kazi na asiyefanya kazi
hana sababu ya kula,kama yalivyo maandishi ya kiroho,” alisema Askofu Kilaini.
Rais yuko mkoani Kagera kwa ziara
yake ya siku mbili mkoani hapa pamoja na shughuli zingine atakagua miradi mipya
inayojengwa na kuweka mawe ya msingi ambayo ni Shule ya sekondari ya Ihungo na
zahanati ya Kabyaile ambazo ziliharibiwa na tetemeko la ardhi na kuzungumza na
wananchi wa Kagera.
No comments:
Post a Comment