![]() |
| Daraja la Kigamboni |
Uchaguzi wa kumpata Meya wa Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es
Salaam, umefanyika na hatimaye Diwani wa Kata ya Pemba Mnazi kutoka
Chama cha Mapinduzi (CCM), Maabadi Hoja amechaguliwa kuwa Meya wa kwanza.
Uchaguzi huo ulifanyika jana kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni, Rahel Mhando, ambaye alikuwa
msimamizi wa uchaguzi, alisema mgombea huyo wa CCM ndiye aliyeshinda.
Washiriki wengine walitoka vyama vya CCM, Chama cha Wananchi (CUF) na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Mhando alisema Hoja alipata
kura tisa dhidi ya Celestine Maufi (CUF) aliyepata kura tano na kura
moja iliharibika.
Pia, Mhando alisema katika uchaguzi huo, Amini Sambo ambaye ni Diwani
wa Kata ya Kibada, pia kutoka CCM, alishinda nafasi ya Naibu Meya,
akipata kura 10 dhidi ya Ernest Mafimbo wa CUF, aliyepata kura tano.
“Tunashukuru uchaguzi umefanyika vizuri Kigamboni, sasa tumepata Meya na
Naibu Meya,” alisema Mhando.
Uchaguzi wa Meya na Naibu wake kwa upande wa Kigamboni, umefanywa baada
ya Wilaya ya Temeke kugawanywa na kuwa wilaya mbili za Temeke na
Kigamboni.
Mhando alieleza kuwa uchaguzi huo ambao ni wa mara ya kwanza kwa
halmashauri hiyo, ulifanyika kwa amani bila kuwapo na malalamiko.

No comments:
Post a Comment