SERIKALI ya Jamhuri ya Korea imetoa
msaada wa Dola za Marekani 50,000 (Sh milioni 105) za kwa ajili ya waathirika
wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu.
Msaada huo ulikabidhiwa Dar es Salaam
jana na Balozi wa Korea nchini, Song Geum Young na kupokewa na Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga kwa niaba ya
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Baada ya kupokea msaada huo, Dk
Mahiga aliishukuru Serikali ya Korea na kuahidi msaada huo ataukabidhi kwa
Waziri Mkuu ili uweze kutumika kama ulivyokusudiwa. Alisema Korea imekuwa mbia
mkubwa wa Tanzania tangu nchi hiyo ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Tanzania
miaka 25 iliyopita.
Alieleza katika kipindi hicho
Tanzania imekuwa ikipokea misaada mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na ya
kibinadamu ukiwemo msaada huo wa fedha uliolekezwa kwa waathirika wa tetemeko
la ardhi la mkoani Kagera.
Waziri huyo alitaja misaada ambayo
Korea imeipatia Tanzania kuwa ni pamoja na ujenzi wa daraja la Malagarasi
mkoani Kigoma, ujenzi wa hospitali ya kisasa ya Mloganzila wilayani Kinondoni,
Dar es Salaam na ujenzi wa hospitali ya uchunguzi wa afya ya Mama iliyopo
Chanika, Ilala, Dar es Salaam.
Naye Balozi wa Korea nchini aliahidi
kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania hususan kutoa misaada ya
maendeleo ili iweze kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
No comments:
Post a Comment