SERIKALI imesema vijiji vyote ambavyo
havijafikishiwa huduma ya umeme vitapata huduma hiyo kupitia mradi mkubwa wa
umeme vijijini Awamu ya Tatu unaotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA),
unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo katika ziara yake mkoani Mara
ya kukagua utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini awamu ya pili (REA II) ambao
unamalizika.
Katika maeneo mbalimbali
aliyotembelea Muhongo, alielezwa kuwa vijiji vya ndani havina umeme kwani
nishati hiyo imeishia kwenye vijiji vilivyopo katika barabara kubwa na kwenye
vituo vya biashara.
Alisema serikali inatambua vijiji
ambavyo havikufikishiwa huduma hiyo, hivyo aliwaasa wananchi katika vijiji
hivyo kuwa na subira kwani lengo la serikali ni kuhakikisha ndani ya miaka 10
vijiji vyote nchini viwe vimefikiwa na umeme.
Alisema mradi wa REA III umetengewa
zaidi ya Sh trilioni moja ambayo ni mara tatu zaidi ya iliyotengwa katika mradi
wa REA II ambao unamalizika kwa kuunganisha baadhi ya vijiji.
Aliongeza kuwa sasa serikali ipo
katika utaratibu wa kuwapata wakandarasi mahiri ambao watakabidhiwa jukumu la
kutekeleza mradi huo ambao ni mkubwa.
Akizungumzia mradi huo wa REA III,
Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Shirika la Umeme (Tanesco), Amos Maganga, alisema
mbali na kuunganisha vijiji vyote, pia mradi huo umelenga kuhakikisha unamaliza
mapungufu yaliyojitokeza katika REA II.
Alisema katika utekelezaji wa mradi
wa REA II kuna mapungufu yaliyojitokeza kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwa
na wigo mpana, hivyo kusababisha baadhi ya vijiji kurukwa, vingine kutofikiwa na
vilevile uhaba wa baadhi ya vifaa katika maeneo mbalimbali.

No comments:
Post a Comment