Habari motomoto zilizojili hivi punde kutoka kila kona ya Dunia

Wednesday, 28 December 2016

MAJI YAPUNGUA KATIKA BWAWA LA MINDU MKOANI MOROGORO





MABADILIKO ya tabia nchi yaliyosababisha kukosekana kwa mvua za kutosha, kumefanya kupungua kwa kiwango cha ujazo wa maji kwenye bwawa la Mindu linalohudumia maji safi kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro, imeelezwa.

Mbali na mabadiliko hayo ya tabia nchi, pia uharibifu wa mazingira kwenye safu ya milima ya Uluguru, uchepushaji wa maji kwa shughuli za kilimo cha mboga katika vyanzo vya maji kumesababisha kupungua kwa maji katika bwawa hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika Manipaa ya Morogoro (Moruwasa), Nicholaus Angumbwike, alisema hayo hivi karibuni wakati akitoa taarifa ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe.
Naibu Waziri huyo yupo katika mkoa wa Morogoro akiendelea na ziara ya kukagua miradi ya maji, ambapo pia alitembelea bwawa la Mindu na vyanzo vingine vya maji katika manispaa hiyo kabla ya kuendelea wilaya nyingine za mkoa huo.
Angumbwike alisema katika taarifa yake kuwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro watakuwa hatarini kukosa huduma ya maji safi na salama kutokana na chanzo cha maji bwawa la Mindu kinachotegemewa na asilimia 80 kuendelea kupungua.
Alisema bwawa hilo kwa sasa limepungua mita za ujazo 504 ambalo kwa wastani linatakiwa liwe na mita za ujazo 507 kutoka usawa wa bahari, ili kuendelea kutoa huduma za maji kwa wakazi wa manispaa hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema kama mvua hazitanyesha kwa miezi miwili ijayo akiba ya maji iliyopo kwenye bwawa hilo itaisha, hivyo mamlaka italazimika kuzima mitambo ya kusukuma maji.
Hata hivyo, alisema ili kuweza kuhifadhi kiwango cha ujazo kinachotakiwa kwa sasa huduma ya maji katika Manispaa ya Morogoro imekuwa ikitolewa kwa mgawo. Pamoja na hayo, alivitaja vyanzo vingine vya maji ni vya mseleleko kikiwemo cha Mambogo na Vituli ambavyo vimekauka.
Alisema vyanzo hivyo vinatoa asilimia 20 ya maji yanayotumiwa na wananchi na kutokana na uhaba huo baadhi wanalazimika kutumia maji ya visima ambayo si safi na salama kwa afya zao.
Naye Ofisa wa Bonde wa Wami – Ruvu, Praxeda Karugendo, alisema kupungua kwa maji katika bwawa la Mindu kunatokana na tabia ya uchepushaji wa maji kwenda kwenye mashamba unaofanywa na watu wanaolima jirani na mito inayoingiza maji katika bwawa hilo.
Hata hivyo, alizitaja sababu nyingine ni uharibifu wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kukata miti kwenye vyanzo vya maji pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, ambapo majira ya mvua yamekuwa yakibadilika kila mwaka.
Kutokana na hali hiyo, Kamwelwe alimuagiza ofisa huyo kufanya kazi ya kuwaondoa watu wanaoishi na kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kwenye mito.
Pamoja na agizo hilo, Naibu Waziri huyo alipiga marufuku tabia ya kuchepusha maji kiholela kwa ajili ya kumwagilia bustani za mboga.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo alisema, serikali inaendelea na mchakato wa kuboresha miundombinu ya maji ukiwemo upanuzi wa bwawa la Mindu ili liweze kuhifadhi maji mengi zaidi.





No comments:

Post a Comment