WATU wawili wamekufa huku wengine
wanne wakijeruhiwa baada ya majambazi walio na silaha kuvamia mgodi wa dhahabu
wa Nholi uliopo wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.
Majambazi hao wanadaiwa kupora
dhahabu, fedha na mali nyingine na kuwavua watu nguo na kuondoka nazo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk
Charles Kiologwe alikiri kupokelewa kwa miili ya watu wawili hospitalini hapo
na majeruhi wanne.
Alisema mwili mmoja upo katika hali
mbaya. Waliofariki dunia katika tukio hilo, walitajwa kuwa ni Lukumale Membo na
mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Hamisi.
Kwa mujibu wa Muuguzi Msaidizi wa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Melisiana Danford, maiti hao na majeruhi
walipokelewa hospitalini hapo saa 6 usiku kuamkia jana mara tu baada ya kutokea
kwa tukio hilo. Majeruhi katika tukio hilo ni Sunday Undi (49), Lawrence
Mhagama (35) , Maila Mchele (44) na Sophia Sayuni (37).
Wakizungumza katika wodi namba moja
ambako wamelazwa, majeruhi hao walisema walivamiwa na majambazi, ambao baadaye
waliwapiga risasi na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine kujeruhiwa.
Lawrence Mhagama ambaye amepigwa
risasi mguu wa kushoto, alisema amekuwa akiendesha shughuli za uchimbaji mdogo
kwenye mgodi huo. Alisema siku ya tukio majira ya saa mbili usiku akiwa ndani,
alisikia milio ya risasi nje na alipojaribu kutoka, alipigwa risasi ambayo
ilimjeruhi mguuni.
“Chanzo cha tukio kwa kweli sikijui
ila majambazi walituvamia , mimi ni mgeni eneo hilo nilikwenda kwa ajili ya
kazi ya mgodi, nimepigwa risasi mguuni ambapo mpaka sasa bado ninayo mwilini,
wanasema wataniruhusu nikipata nafuu na baadaye wataangalia uwezekano wa kuitoa
risasi hiyo,” alisema.
Alisema majambazi hao, walipora mali
nyingi ambapo waliwavua watu nguo na kuondoka nazo huku wakiacha watu uchi.
Majeruhi mwingine aliyelazwa wodi
namba moja, Sunday Undi, alisema walivamiwa na majambazi hao majira ya saa
mbili kasorobo usiku wa kuamkia juzi, wakiwa kwenye kioski cha Maila Mchele,
wakipata vinywaji na kuendelea na mazungumzo.
“Tulivamiwa tukasikia tunaambiwa tuko
chini ya ulinzi, kwa vile lilikuwa ni tukio la kushtukiza tukawa tunashangaa,
wakapiga risasi juu ikabidi tuingie ndani ya kibanda kile baada ya muda
tukajikuta watu saba tukiwa chini ya kitanda,” alisema.
Alisema majambazi hao waliwaamrisha
watoke na kuwaambia kila mtu atoe alichonacho na aliyekuwa akikataa, aliamriwa
kuvua nguo.
“Walininyang’anya fedha na simu,
wakatuvua na suruali wakaondoka nazo, mimi binafsi wamenipora Shilingi milioni
mbili nilizokuwa nazo,” alisema.
Alisema majambazi hao walikuwa zaidi
ya wanne na walikuwa wamevalia kininja. Alisema mtu aliyejaribu kuwatazama
usoni, alikuwa akipigwa risasi. Majeruhi mwingine katika tukio hilo, Maila
Mchele ambaye amelazwa wodi hiyo akiwa hajitambui, amejeruhiwa vibaya.
Inadaiwa alipigwa risasi tumboni na
kutokea upande wa pili. Majeruhi wa nne, Sophia Sayuni (37) amelazwa wodi namba
10 hospitalini hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma,
Lazaro Mambosasa alipohojiwa kuhusu tukio hilo, alisema atalitolea ufafanuzi
baadaye.

No comments:
Post a Comment