HALMASHAURI ya Wilaya ya Bariadi
mkoani Simiyu, imeanza msako wa kuwatembelea walengwa wanaonufaika na Mfuko wa
Jamii (TASAF) Awamu ya Tatu.
Zaidi ya watu 80 wamekamatwa na
kufikishwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Bariadi kwa kudaiwa kufisadi fedha
hizo.
Akizungumzia hilo mbele ya waandishi
wa habari ofisini kwake jana, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Abdallah Malela
alisema kuwa jumla ya kaya 80 katika halmashauri hiyo, zinatafutwa ili
zirejeshe fedha zote.
Alisema imebainika kuwa kaya 80
ziliingizwa katika mradi wa TASAF III kwa njia za kinyemela na kuchukua Sh
milioni 17.8.
“Ni kweli kuna msako huo, jumla ya
kaya 80 hazikustahili kuwemo katika mpango huu, tulifanya ukaguzi mpya baada ya
maelekezo kutoka Serikali Kuu kututaka kupitia upya walengwa, kama wanakidhi
vigezo vya kuwemo kwenye mpango,” alieleza Malela. Alisema kaya hizo
zilibainika kutokuwa na vigezo.
Ziliandikiwa barua tangu Agosti mwaka
huu, kutaka warejeshe fedha zote za miezi sita zilizotolewa kwao. Alieleza kuwa
baada ya kupatiwa barua hizo, hakuna kaya hata moja ambayo imeanza kurejesha
fedha hizo.
Hali hiyo imesababisha kuwepo kwa
msako huo wa nguvu. Alisisitiza kuwa wahusika hawatapewa dhamana mpaka
warejeshe fedha zote.
“ Watu ambao tumewakamata hawapewi
dhamana mpaka warejeshe fedha za serikali. Mpaka leo tumefanikiwa kurejeshewa
kiasi cha Shilingi milioni 1.1 kati ya milioni 17.8,” alieleza Malela.
Alisema msako huo utaendelea kwa
halmashauri nzima mpaka pesa zote zirejeshwe, ili kuweza kutumika kwa walengwa
ambao walikusudiwa katika mpango huo.
“ Leo ni siku ya tatu tunahangaika
kupata dhamana, mama yetu amekamatwa, wamesema ili kupata dhamana mpaka
arejeshe kiasi chote ambacho amepokea. Tangu aanze kuchukua fedha za TASAF
anadaiwa shilingi 240,000,” alisema mmoja wa mtoto wa mnufaika, ambaye hakutaka
kutaja majina yake.
Mwenyekiti wa mtaa ambaye hakutaka
kutaja jina lake, alisema kuwa wao kama viongozi wa mtaa waliletewa barua
kutoka TASAF wilaya, yenye majina ya watu ambao walikuwa kwenye mpango huo na
wanatakiwa kurejesha fedha zote kutokana na kutokidhi vigezo.
“ Nilipokea barua ikiwa na majina ya
watu wanaotakiwa kurejesha fedha zote walizochukua toka waanze kupokea,
wanasema wao hawakustahili kuwemo katika mpango huo, wengi wanadaiwa zaidi ya
shilingi 200,000”
alisema Mwenyekiti huyo.
No comments:
Post a Comment