RAIS John Magufuli amekabidhi msaada
wa vyakula mbalimbali na juisi kwa kituo cha wazee wasiojiweza (SILABU) cha
mjini Kigoma ikiwa ni kutoa mkono wa sikukuu kwa watu wasiojiweza.
Msaada huo umekabidhiwa kwa wazee hao
kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa Kigoma, Emmanuel Maganga.
Alisema msaada huo umetolewa
kuwawezesha wazee hao kusherehekea sikukuu ya Krismasi sawa na watu wengine
wenye uwezo.
Miongoni mwa vyakula vilivyokabidhiwa
ni pamoja na kilo 90 za mchele, mafuta ya kula ndoo tatu na mbuzi mmoja kwa
ajili ya kitoweo.
Maganga naye alitoa katoni tano za
juisi na miche 24 ya sabuni. Mwenyekiti wa kambi hiyo, Hamisi Sabuni
amemshukuru Rais Magufuli kwa msaada huo, akisema tangu aingie madarakani
ameonesha dhamira ya dhati ya kuwajali watu wasiojiweza na wenye kipato duni.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Mfawidhi
wa Mkoa Kigoma, Heradius Mushi alisema pamoja na serikali kutoa fedha kwa ajili
ya kugharamia chakula kituoni hapo, bado kiasi cha fedha kinachotolewa
hakikidhi mahitaji na kuomba wahisani zaidi wajitokeze si tu nyakati za
sikukuu, bali mara kwa mara.

No comments:
Post a Comment