WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema
Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano na Serikali ya China katika nyanja
mbalimbali kupitia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, nishati na miundombinu.
Hii ni kauli aliyoitoa hivi karibuni, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa
China, Wang Yi, kwa niaba ya Rais John Magufuli, jijini Dar es Salaam.
Majaliwa anataja ushirikiano wa
Tanzania na China kuwa ni wa kihistoria ambao utaendelezwa kwa manufaa ya
wananchi wa pande zote.
Anawakaribisha wawekezaji kutoka
China kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini hususani kwenye miundombinu,
viwanda, kilimo na nishati.
“Tanzania iko tayari kupokea kampuni
zaidi za China kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini,” anasema waziri
mkuu akisisitiza kuwa, nchi iko tayari kupokea viwanda kati ya 200 hadi 700
katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Waziri huyo wa China, Wang Yi
anapongeza utendaji kazi wa Rais Magufuli pamoja na viongozi wengine hususan
katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ambayo matunda yameanza kuonekana.
“Serikali ya China kwa sasa iko
katika mkakati wa kuhamishia viwanda vyake vingi barani Afrika. Iliamua
kuichagua Tanzania kuwa moja kati ya nchi watakazohamishia viwanda hivyo
kutokana na kuridhishwa na dhamira inayoonyeshwa na serikali katika kuleta
maendeleo,” anasema waziri huyo.
Wang alisema China inatambua mchango
mkubwa wa Tanzania katika harakati za kujikomboa hivyo itaendelea kuiunga mkono
kuhakikisha inafikia uchumi mzuri.
Lakini pia, nchi hiyo inasisitiza kuendeleza
ushirikiano wake na Tanzania kwa kuboresha miundombinu ikiwemo kujenga uwanja
wa ndege na bandari Zanzibar.
Pia itajenga jengo la wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mjini Dodoma kuwezesha ihamie mjini
humo kama ilivyoelekezwa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga anasema msaada huo wa China ni
mwendelezo wa ushirikiano ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo Hayati
Mwalimu Julius Nyerere na Mao tse tung. Balozi Mahiga anasema, miradi mingine
itakayotekelezwa ni pamoja na bandari ya Bagamoyo na reli ya Mamlaka ya Reli
Tanzania na Tambia (Tazara).
Kwa mujibu wa waziri Mahiga, kwa sasa
wanaangalia hali ilivyo na fursa zilizopo pamoja na kutazama maeneo mapya ya
kiuchumi na kuyaendeleza.
Mkakati wa China wa kuhamishia
viwanda Afrika, hususani Tanzania, unatoa changamoto kwa serikali na wadau
wengine kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri yatakayofanikisha lengo hilo.
Hii ni pamoja na kuhakikisha, nchi
inakuwa na miundombinu rafiki itakayofanikisha lengo la usafirishaji wa
malighafi na huduma nyingine kwa ajili ya viwanda.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa anasema ndiyo maana serikali imeelekeza bajeti
kubwa kwenye miundombinu kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa viwanda.
"Tumesikia katika semina hii
kwamba wenzetu Wachina wameichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza kutekeleza
mpango wake wa kuhamishia viwanda barani Afrika, hii ni fursa nzuri kwetu
ambapo kama serikali tumeamua kutenga zaidi ya asilimia arobaini ya bejeti
kwenda kwenye miundombinu kwa ajili ya kuchochea kasi ya uanzishaji wa
viwanda," ni kauli ya Profesa Mbarawa aliyoitoa mwaka jana katika semina
ya kimataifa, iliyoandaliwa na ubalozi wa China nchini.
Kupitia miundombinu bora, kutakuwa na
kasi ya uanzishwaji wa viwanda kwani wakulima watapata urahisi wa kusafirisha
mazao yao sambamba na kuwa na uhakika wa bidhaa kufika sokoni na hivyo hivyo
kwa malighafi kwenda viwandani.
Lakini pia nishati ya umeme yenye
uhakika, ni eneo lingine linalohitaji kufanyiwa kazi ipasavyo katika mchakato
wa kukaribisha viwanda hivyo. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo amekuwa akisisitiza juu ya hilo kwa kusema, ili Tanzania iweze kuwa
nchi ya viwanda, nishati ya uhakika inahitajika.
Kutokana na fursa ya gesi nchini,
Waziri Muhongo amekuwa akihimiza kampuni kuwekeza katika uzalishaji wa umeme
unaotokana na gesi.
Miongoni mwa maeneo yanayohitaji
uwekezaji katika kuzalisha umeme kwa kutumia gesi ni pamoja na Mtwara, Lindi,
Somanga Fungu, na Mkuranga.
Msimamo wa Profesa Muhongo ni kwamba,
hakuna nchi duniani iliyopiga hatua kimaendeleo bila kuwa na nishati ya uhakika
ya umeme.
Hatua ya hivi karibuni ya Waziri
Muhongo kuzuia Shirika la Umeme (Tanesco) kupandishwa kwa bei ya umeme, ni
uthibitisho wa nia ya serikali kuhakikisha mikakati ya kujenga viwanda
inatekelezeka. Rais John Magufuli ambaye amepongeza hatua hiyo ya kusitisha
kupanda kwa bei ya umeme, anafafanua zaidi akisema, haiwezekani kupanga
mikakati ya kujenga viwanda wakati umeme ukipanda.
“Namshukuru sana Waziri wa Nishati na
Madini kwa maamuzi ya kusitisha hayo, kwa hiyo umeme hakuna kupanda
bei,haiwezekani unapanga mikakati ya kujenga viwanda…,” Rais Magufuli alisema
hayo kwenye ibada ya mwaka mpya, katika kanisa kanisa la Bikira Maria Mama Mwenye
Huruma, Kanisa Kuu Jimbo Katoliki la Bukoba, mkoani Kagera.
Ikiachwa viwanda ambavyo China
itavielekeza nchini, pia vipo vinavyohitaji kufufuliwa ambavyo ukuaji na ustawi
wake unategemea kwa kiwango kikubwa uwapo wa miundombinu pamoja na nishati ya
uhakika ya umeme.
No comments:
Post a Comment