KAMA ingekuwa ni muziki wa msanii wa
kizazi kipya Darasa ungesema wacha maneno weka muziki lakini kwa vile ni mpira,
unaweza sema wacha maneno weka Simba kaua Yanga.
Hiyo ni kutokana na Simba jana
iliendeleza ubabe kwenye uwanja wa Amaan mjini hapa baada ya kuifunga Yanga kwa
mikwaju ya penalti 4-2 katika mechi ya nusu fainali za kombe la Mapinduzi.
Ushindi huo unaifanya Simba kushinda mara nne kati ya mara tano alizokutana na
Yanga kwenye uwanja huo.
Miamba hiyo ya soka ilikwenda kwenye
mikwaju ya penalti baada ya mechi kuisha kwa sare ya bila kufungana katika
dakika 90 za mchezo. Jonas Mkude alikuwa wa kwanza kupiga mkwaju wa penalti kwa
timu yake ya Simba ambapo alipata kabla Kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ wa Yanga
kukosa mkwaju wake baada ya kipa wa Simba Daniel Agyei kupangua.
Agyei alipiga penalti ya pili kwa
Simba ambapo alipata huku Method Mwanjali akikosa, Muzamiru Yassin na Bukungu
walipata penalti zao na kwa upande wa Yanga Simon Msuva na Thabani Kamusoko
walifunga huku Haji Mwinyi akikosa. Kwa ujumla mechi hiyo haikuwa na ufundi na
ilitawaliwa na rafu za hapa na pale huku timu zikishambuliana kwa zamu katika
kila kipindi.
Ni Simba ndio walionza kugongeana
vizuri katika dakika ya saba lakini beki Kelvin Yondani akaokoa hatari hiyo.
Dakika moja baadae Haruna Niyonzima alipata nafasi nzuri na kupiga shuti
lililodakwa vizuri na kipa wa Simba Daniel Agyei.
Simon Msuva alikosa bao katika dakika
15 baada ya kuunganisha pasi ya Amisi Tambwe na dakika ya 36 Jamvier alikoa
mpira uliokuwa ukielekea golini mwa Simba huku tayari kipa Agyei akiwa
‘ameshapotea’.
Zikiwa zimesalia dakika mbili kabla
ya kipindi cha kwanza kumalizika, Mohamed Ibrahim ‘Mo’ nusura aifungie Simba
bao lakini mpira aliopiga uligonga mwamba wa juu na kumkuta Shiza Kichuya
ambaye alipiga na mpira ukatoka nje. Kipindi cha pili kilianza kwa taratibu
kama ilivyokuwa cha kwanza na wachezaji wa timu zote wakionekana kusubiri
kwenda kwenye penalti.
Yanga imepata kipigo hicho baada ya
kufungwa mabao 4-0 katika mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya Azam. Kwa matokeo
hayo, Simba sasa itacheza fainali za michuano hiyo dhidi ya Azam keshokutwa.
Azam ilikuwa ya kwanza kutinga fainali baada ya kuifunga Taifa Jang’ombe bao
1-0 lililofungwa na Frank Domayo kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa
Jang’ombe Ahmed Ally katika dakika ya 33.
Yanga walifulia jana
ReplyDelete