Charles Mkumbo, Kamanda wa Polisi Arusha
FAMILIA jijini hapa
inadaiwa kumzika kwa siri mtoto wao mdogo wa kike wa miaka mitatu katika kaburi
lililofichwa, huku majirani wakidanganywa kuwa binti huyo yupo hai.
Taarifa za kisa
hicho cha kusikitisha zimevifikia vyombo vya usalama. Kwa sasa kuna mipango ya
kuhakikisha kuwa mwili wa binti huyo, Nuru Losipha aliyezikwa kwa siri na
familia yake, unafukuliwa kwa uchunguzi zaidi.
Inadaiwa kuwa
Losipha alipoteza maisha wakati akifanyiwa tohara au ukeketaji na ngariba,
ambaye jina lake halikufahamika mara moja, huku familia yake ikishuhudia.
Kitendo hicho
kilifanyika katika kijiji cha Engutoto Kata ya Mwandeti wilayani Arumeru
Desemba 28, mwaka jana, zikiwa zimebaki takriban siku tatu tu, kabla ya mtoto
huyo aliyekuwa na umri wa miaka mitatu tu, hajaingia mwaka mpya wa 2017.
Mtendaji wa Kata ya
Mwandeti, Njivaini Kivuyo awali alikuwa amepitwa na taarifa hizo hadi vyombo
vya habari vilipotinga kijijini hapo kwa uchunguzi na ndipo alipolazimika
kwenda kuripoti tukio hilo kwenye kituo cha Polisi cha Ngaramtoni.
Kamanda wa Polisi
mkoani hapa, Charles Mkumbo aliapa kuwa liwalo na liwe na kwamba ikiwezekana
kaburi litafukuliwa ili mwili wa malaika huyo asiye na hatia, uchunguzwe upya.
“Ndio kwanza
nazipata hizi taarifa, na kama polisi tutaomba kibali cha mahakama ili twende
kulifukua kaburi husika tujiridhishe kama kweli mtoto huyo amezikwa humo na
iwapo tutaukuta huo mwili, basi tutaanza uchunguzi juu ya kifo chake,” alisema
Kamanda arles Mkumbo.
Baba wa marehemu,
Losipha Kaiser anadai kuwa mtoto wake alifariki kutokana na ugonjwa wa baridi
yabisi na kwamba aliugua kwa kipindi kirefu kabla ya kupoteza maisha Desemba
28, mwaka jana. Lakini madai yake hayo yanapingana na ripoti ya muuguzi katika
duka la dawa lililopo kijiji cha jirani cha Kidali, anayeitwa Jane Andrew.
“Walimleta mtoto
hapa walitaka nimsaidie tiba, lakini tayari huyo binti alikuwa amezimia na
kutokwa na damu nyingi,” alidai.
Muuguzi huyo aliwahimiza
wamkimbize mtoto hospitali, na hakufahamu nini kiliendelea hadi ripoti za kifo
zilipomfikia.
Huku serikali
ikipiga marufuku vitendo vya ukeketaji kwa wasichana, bado kuna familia nyingi
kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa, zinaendeleza mila hiyo kwa
siri.
Kwa sasa familia
hizo zimegundua mbinu mpya ya kuwatahiri watoto wa kike wakiwa wadogo sana,
kuepuka kukamatwa.
Ngariba wanaotumika
kukeketa watoto, mara nyingi ni akina mama vikongwe wasiokuwa na ujuzi, taaluma
za afya na hutumia vifaa butu, ambazo husababisha uvujaji mwingi wa damu na
kuwa chanzo cha maambukizi ya magonjwa mengine.
No comments:
Post a Comment