WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepiga marufuku na kufuta posho
zilizo nje ya utaratibu na zisizotambulika kisheria.
Posho hizo ni za posho za mazingira magumu, kujenga uwezo na
vitafunwa katika halmashauri za wilaya na manispaa zote nchini. Badala yake,
ametaka posho hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo.
Kutokana na agizo hilo, kwa jiji la Dar es Salaam pekee
zaidi ya Sh bilioni 130 zilizokuwa zikilipwa kwa halmashauri na manispaa za
jiji hilo kwa posho mbalimbali, zitaokolewa na kuingizwa kwenye miradi na
shughuli za maendeleo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu huyo ametoa siku tatu kwa
watumishi wa umma 10, wanaotakiwa kuripoti katika halmashauri na manispaa mpya
ya Kinondoni, kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi. Vinginevyo, watakuwa
wamejifukuzisha kwenye utumishi wa umma.
Alisema hayo alipozungumza na watumishi wa Halmashauri na
Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam jana katika ziara yake ya siku moja
ya kujitambulisha na kukumbushana kuhusu uwajibikaji. Majaliwa aliitaka kila
halmashauri hiyo, ifanye tathmini ya mahitaji ya kila kata na kusimamia
maendeleo.
Alisema katika halmashauri kumekuwa na matumizi ya fedha
nyingi kinyume na taratibu na kanuni. Matumizi hayo huwanufaisha wachache, huku
wengine ambao nao waliwajibika wakinyimwa fursa ya kunufaika na wao.
“Utakuta hadi mlinzi anahangaika katika suala zima la
ukusanyaji wa mapato ya halmashauri, lakini mwisho wa siku vitafunwa huliwa na
wachache wanaojiita wakubwa huku wengine wakisikilizia kwa nje,” alisema.
Alitolea mfano manispaa za Ilala, Temeke na Ubungo kuwa
kiasi cha fedha za posho kinacholipwa kwa ajili ya vitafunwa kwa mwaka ni Sh
milioni 600, pamoja na posho za mazingira magumu jumla ni Sh milioni 960 kwa
kila manispaa.
Kwa upande wa Kinondoni, alisema manispaa hiyo pamoja na vitafunwa
ambavyo ni zaidi ya Sh bilioni moja kwa mwaka, pia hulipa posho ya nyuma kwa
wakuu wa vitengo kwa mwaka ambayo ni Sh bilioni 2.8.
“Nafuta hizi posho zote ambazo hazitambuliki kisheria,
naagiza kuanzia leo malipo haya yapelekwe kwenye shughuli za maendeleo. Naonya
Mkurugenzi yeyote nitakayebaini amelipa watu wake posho hizi, amejifukuzisha
kazi mwenyewe,” alisisitiza.
Aidha, aliagiza kuwa kiasi cha Sh 800,000 kinachotolewa kwa
kila diwani kwa ajili ya kufanya uhamasishaji wa maendeleo kwenye kata yake,
kuanzia sasa kisitolewe moja kwa moja kwa diwani, bali kipelekwe kwenye kata na
kufuatiliwa namna kinavyotumika.
Pamoja na hayo, Waziri Majaliwa alionya halmashauri zote
kuhakikisha kuwa kila fedha inayopelekwa kwenye halmashauri hizo, inatumika
kama ilivyokusudiwa. Endapo itabainika kutumika kwa shughuli nyingine, wahusika
watachukuliwa hatua.
“Narudia nataka hili lieleweke,kila fedha itakayopelekwa kwa
halmashauri itumike kwa lengo lililokusudiwa. Kama ni fedha ya ujenzi wa
madarasa iende kwenye ujenzi wa darasa na uendane na thamani ya fedha yenyewe
na si vinginevyo,” alisema.
Pamoja na hayo, Kiongozi huyo pia alibainisha kuwa serikali
ya awamu ya tano, haitambeba tena mtumishi wa umma yeyote, anayevunja maadili
ya utumishi wa umma au anayekosa nidhamu kwa kumhamisha kituo, bali kuanzia
sasa mtumishi huyo atafukuzwa kazi.
Aliwataka watumishi wote wa umma nchini, kuwajibika ipasavyo
kwa kuhakikisha wanamtumikia vyema mwananchi, ikiwa ni pamoja na kuepuka
vishawishi na kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa.
“Juzi nilipokuwa Longido, nilikuta mtumishi mmoja
amesababisha hasara ya takribani Shilingi bilioni 1.2. Baada ya kujua
ameharibu, akaomba uhamisho wa kwenda Bahi, tukamzuia, sasa hili ni fundisho,
serikali haimbebi tena mtu anayeharibu kazi yake. Hapohapo ulipoharibu ndio
tunapomalizana,” alifafanua.
Kuhusu maslahi ya watumishi wa umma, Waziri Majaliwa alisema
serikali imejipanga kuboresha maslahi ya watumishi wote wa umma na ndio maana
imeunda timu maalum, kwa ajili ya kuhakiki viwango vya mishahara vinavyotolewa
ili kujua kama vinaendana na hali ya maisha.
Aidha, alisema serikali hiyo pia inataka kuondokana na
tatizo la malimbikizo ya fedha za watumishi wake, kwa kulipa malimbikizo yote
yanayodaiwa na watumishi.
Akizungumzia suala la kupokelewa na mabango ya wananchi kila
anapokwenda, Majaliwa alisema kuanzia sasa popote atakapoenda, akikutana na
mabango, kiongozi yanayomhusu ajiandae kumpatia majibu, kwa kuwa hiyo ni alama
ya kutowajibika kwake.
“Ukiona nimepokewa na mabango wewe kama ni kiongozi yasome
mapema ujipange kunipa majibu, maana hii ni indication kuwa watu hawathamaniwi
mpaka wamsubiri waziri Mkuu ndipo wasikilizwe. Tatueni kero za wananchi wenu
kabla hawajanifikia,” alionya.
Akizungumzia watumishi 10 walioshindwa kuripoti katika vituo
vyao vya kazi katika halmashauri na manispaa ya Kigamboni, Majaliwa alisema
kitendo cha watumishi hao, kushindwa kuripoti bila kutoa taarifa ni dalili kuwa
hawataki tena kuwa watumishi wa umma.
“Nawapa siku tatu waripoti wenyewe kabla hawajiachisha kazi,
na kama kuna mtu anawazuia awaachie mara moja,” alisema Majaliwa.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa wakati
akiwasilisha taarifa ya wilaya hiyo, alibainisha kuwa mpaka sasa takribani
asilimia 98 ya watumishi wa umma waliotakiwa kuhamia kwenye halmashauri hiyo
wameripoti kazini isipokuwa watumishi hao 10 ambao hakuna taarifa zozote juu
yao.
No comments:
Post a Comment