MKOA wa Mwanza umefanya kazi kubwa ya kukamilisha ujenzi wa
miradi mikubwa ya maji vijijini katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Karibu maeneo yote ya miji mikuu ya wilaya, wananchi wake wanapata huduma ya
maji safi na salama.
Mhandisi wa Maji wa Mkoa wa Mwanza, Warioba Sanya, anasema,
hadi Septemba mwaka jana, maeneo ya pembezoni mwa jiji wanaopata maji ni
asilimia 51 na maeneo ya mijini kati ni asilimia 77.
Katika mahojiano , Sanya ambaye kitengo chake kinawakilisha
wizara na mkoa katika utoaji wa huduma za maji mijini na vijijini, anaeleza namna
utekelezaji wa miradi ya maji unavyofanyika.
Mhandisi huyu wa maji ambaye anasema anawajibika kumshauri
Katibu Tawala wa Mkoa katika suala zima la utekelezaji wa ya maji, anasema mkoa
wa Mwanza una jumla ya vyanzo vya maji 3,372 vya maji. Kati ya hivyo, vyanzo
2,399 ndivyo vinavyofanya kazi na 933 sawa na asilimia 28, havifanyi kazi
kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kukauka.
“Juhudi zinazofanywa na mkoa kwa sasa ni kuhamasisha jamii
kuhakikisha kuwa zinalinda vyanzo vya maji kwenye maeneo yao ikiwa ni pamoja na
kulinda na kuhifadhi mazingira,” anasema.
Mtaalamu huyu ambaye miongoni mwa majukumu yake ni pamoja
kutayarisha bajeti ya miradi ya maji ya mkoa, anasema katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita, serikali imetumia sh bilioni 3.7 kwa ajili ya kukarabati
jumla ya miradi ya maji 160 iliyokuwa katika hali mbaya kwa wilaya saba za
Mwanza.
Miradi hiyo imewanufaisha watu 96,103.
Vituo vya maji 227 katika wilaya za Sengerema, Buchosa,
Magu, Mwanza Jiji ( Nyamagana), Misungwi, Kwimba na Ukerewe vinatoa maji safi
na salama. Mhandisi huyu ambaye ndiye mwenye jukumu la kusimamia ujenzi wa
miradi ya maji inayotekelezwa na wakandarasi, anasema miradi iliyotekelezwa
katika kipindi hicho ni miradi ya maji ya bomba 21, visima virefu 19 na matangi
ya kuvuna maji 23.
Mingine ni , visima vifupi 19, vyoo vitano na chemichemi
moja ambayo ilitekelezwa kwa karibu wilaya zote. Miradi hiyo imegharimu
takribani sh milioni 155.7 na kunufaisha jumla ya watu 6,000.
Anaelezea hali ya ukamilishaji wa ujenzi wa miradi ya maji
mijini akisema, serikali imekamilisha ujenzi wa miradi mikubwa yenye thamani ya
sh bilioni 205 itakayowanufaisha jumla ya wakazi 734,149 kwa miji mitatu ya
Ngudu, Nansio na Ukerewe.
Miradi mingine mitatu ya maji ni katika miji ya Misungwi,
Magu na jiji la Mwanza ambayo ipo katika hatua za awali za utekelezaji kwa
ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB). Miradi hii inatoa fursa kwa miji
yote kupata maji ifikapo Juni, 2020 .
Aidha miradi ya maji katika mji ya Misungwi, Magu na jiji la
Mwanza iko katika hatua ya awali ya utekelezaji. Kwa upande wa jiji la Mwanza
kazi inayofanyika kwa sasa ni kujenga chanzo kingine cha kuhifadhi maji
kutokana na chanzo cha Capripoint kushindwa kutoa huduma ya maji kutokana na
ongezeko la idadi ya watu waliopo kwa sasa.
Kuhusu maeneo ya milimani jijini Mwanza yaliyo na uhaba wa
maji , mhandisi huyu anasema serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka
jijini Mwanza(MWAUWASA) imefanikiwa kupanua miundombinu ya maji katika maeneo
hayo.
Anasema pampu ndogo tayari zimefungwa kwa ajili ya kusukuma
maji kwenda maeneo ya Nyasaka-Msumbiji, Lumala, Buswelu, Isamilo, Bugarika,
Nyegezi, Buhongwa, Kitangiri na Capripointi.
“Dhamira ya serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata
huduma ya maji muda wote,” anasema.
Ipo pia miradi ya maji ya vijiji 10 ambayo mhandisi anaelezea kuwa, utekelezaji
wake uko kwenye hatua nzuri ya mafanikio.
Akizungumzia changamoto, mtaalamu huyu anataja kuathirika
kwa visima vifupi vinavyosababishwa na upanuzi wa miji unaofanywa na mamlaka ya
mipango miji.
Chagamoto nyingine ilikuwa ni ya ujenzi wa makazi na
matumizi ya miundombinu ya majitaka ambayo huchafua maji chini ya ardhi.
Lakini pia kuchelewa kwa fedha za maendeleo za usimamizi wa
miradi , ni changamoto inayotajwa kuwa kubwa katika utekelezaji wa miradi ya
maji mijini.
Changamoto nyingine ni kutoanza kujengwa kwa miradi ya maji
inayotoka bomba kuu la Mamlaka ya Kusambaza Maji katika miji ya Kahama na
Shinyanga (KASHWASA) kwenda vijiji vilivyopo ndani ya kilometa 12 vilivyokuwa
vimepangwa kujengewa miradi kupitia programu ya maji vijijini hususani vijiji
vya wilaya ya Misungwi.
Hata hivyo anasema mikakati iliyopo ya kukabiliana na
changamoto hizo kwa sasa ni kuelimisha jamii namna bora ya kulinda vyanzo vya
maji na kuchimba visima virefu visivyoathiriwa na shughuli za mipango miji,
kusimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maji ambayo
haijakamilika.
No comments:
Post a Comment