WAKAZI wa Wilaya ya Bunda mkoani
Mara, wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula, ambapo sasa bei ya mahindi
imepanda. Bei hiyo imetoka sh 14,500 kwa debe moja la mahindi hadi sh 20,000,
mtama sh 10,000 hadi sh 17,500, udaga umetoka sh 12,500 hadi sh 17,500 huku
ulezi ukifikia sh 30,000 kwa debe.
Gazeti hili limebaini hayo katika
uchunguzi wake maeneo mbalimbali pamoja na kwenye masoko wilayani hapa. Bei
hiyo imependa kuanzia Agosti na Septemba mwaka jana na haijashuka hadi sasa.
Baadhi ya wafanyabiashara wa nafaka
kwenye soko kuu la mjini Bunda, katika jimbo la Bunda mjini na kwenye soko la
mji mdogo wa Kibara, katika jimbo la Mwibara, walisema kwa nyakati tofauti
kuwa, bei ya chakula imepanda kutokana na kuwepo upungufu mkubwa wa chakula
katika maeneo hayo.
Walisema kuwa hali hiyo imetokana na
mvua kutokunesha wilayani hapa kwa kipindi kirefu na kusababisha mazao
yaliyokuwa yamelimwa mashambani kukauka na pia wakulima wengine kushindwa
kulima kwa sababu yakuwepo ukame huo.
Walisema kuwa wamekuwa wakiuza
chakula hicho wanachokipata kutoka katika mikoa jirani kwa bei kubwa na kwamba
wao pia ulazimika kukiuza kwa bei hiyo ili waweze kurudisha mtaji wao pamoja na
faida kidogo tu.
Mfanyabiashara katika soko kuu la
Bunda, Esta Samson, alisema kuwa kwa ujumla hali ya chakula katika wilaya
inahitaji tahadhari na kwamba hata biashara yao haiendi kama iwalivyokuwa
wanatarajia.
“Hali ya chakula katika hili soko
letu ni mbaya maana kimepanda sana kutokana na sisi tunavyouziwa kwa bei ya juu
sana. Na hii hali tuseme imeaanza mwezi wa nane na wa tisa mwaka jana. Sasa
hivi gunia moja la mahindi tunalinunua kati ya sh 110,000 hadi sh 120,000,”
alisema Samson.
Baadhi ya wananchi walisema kuwa
wanakabiliwa na njaa kubwa na kwamba hali hiyo inatokana na ukame na pia baadhi
ya mazao yao yaliyokuwa shambani yalishambuliwa na wanyama, wakiwemo tembo
kutoka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
No comments:
Post a Comment