MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu
jijini Dar es Salaam imewakuta na hatia na
kuwahukumu kifungo cha miaka 5 jela au kulipa faini ya Sh milioni 100 kila mmoja vigogo watano waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya rushwa na utakatishaji wa fedha.
kuwahukumu kifungo cha miaka 5 jela au kulipa faini ya Sh milioni 100 kila mmoja vigogo watano waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya rushwa na utakatishaji wa fedha.
Taarifa iliyotolewa na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dar es Salaam jana ilisema kesi hiyo
iliyoendeshwa kwa muda mrefu na kufuatiliwa na watu wengi ilifunguliwa Julai
21, mwaka 2010.
Taarifa hiyo ya Takukuru iliyotolewa
na Ofisa Uhusiano wake Mussa Misalaba iliwataja washtakiwa waliopatikana na
hatia kuwa ni Justice Lumina Katiti aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Mamlaka ya
Mapato (TRA) na Marcus Mussa
Masila aliyekuwa Mhasibu wa Kampuni ya Simu Tanzania TTCL.
Wengine ni Kanuti Ferdinand Ndomba
mfanyabiashara wa Kampuni ya UEE Tanzania Limited, Gidion Wasonga Otullo
mfanyabiashara wa kampuni ya East Africa Procurement Services na Robert Phares
Mbetwa mfanyabiashara kutoka kampuni ya Romos Technology Limited.
Kesi hii iliendeshwa na waendesha
mashtaka kutoka ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) na TAKUKURU ambao
ni Awamu Mbagwa (DPP), Shedrack Kimaro (DPP), Estazia Wilson (DPP) na Marx Ally
(Takukuru).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya
Takukuru, hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama hiyo Januari 17 mwaka huu mbele ya
Hakimu Mkuu Mkazi Renatus Rutatinisibwa baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi
uliotolewa na upande wa mashtaka na hivyo kuwatia hatiani washtakiwa kwa jumla
ya makosa 51 ya rushwa na utakatishaji wa fedha haramu.
Washtakiwa walipelekwa Magereza
kutumikia kifungo cha miaka 5 baada ya kushindwa kulipwa faini hiyo ya Sh
milioni 100.
Ilidaiwa kuwa kati ya mwaka 2007 na
2009 watuhumiwa kwa kushirikiana walikula njama kuchepusha Sh 3,399,251,740.24
za TTCL zilizokusudiwa kulipa kodi TRA
na kulipwa kinyume cha sheria kampuni ya UEE. Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa
mshitakiwa Masila aligushi sahihi za watia sahihi wa TTCL na kubadili fomu za
TIS zilizokusudiwa kupeleka fedha TRA
na kuweka jina la UEE.
Ilidaiwa kuwa mshitakiwa Katiti alionesha
kwenye mfumo wa TRA kuwa TTCL
ilikuwa imelipa kodi zote. Ilidaiwa kuwa kati ya mwaka 2008 na 2009 Katiti ,
Masila, Wasonga na Mbetwa walijipatia mali nyingi na kununua magari ya kifahari
na nyumba kutokana na fedha hizo haramu.
No comments:
Post a Comment