SERIKALI mkoani
Dodoma imeombwa kuingilia kati mgogoro katika soko lisilo rasmi la Rehema
Nchimbi kutokana na malalamiko ya wajasiriamali wanawake kuombwa rushwa ya
ngono sambamba na kulipishwa fedha bila kupewa risiti.
Walitoa malalamiko
yao juzi mbele ya waandishi wa habari muda mfupi baada ya uongozi wa soko hilo
kuwatangazia wafanyabiashara hao kuwa mkutano ambao ulikuwa ufanyike siku hiyo
hautakuwepo, jambo ambalo lilikataliwa na wajasiriamali hao.
Mmoja wa
wajasiriamali katika soko hilo, Prisca Chibwaye alisema baadhi ya viongozi wa
soko wanatumia nafasi zao kunyanyasa wanawake kwa kuwaomba rushwa ya ngono,
huku wakilipishwa fedha bila kutoa risiti kwa madai kuwa malipo hayo ni kwa
ajili ya kuchangia ukarabati wa soko hilo.
Alisema viongozi hao
wamekuwa ni kero kubwa hususan kwa wanawake ambao wamekuwa wakidaiwa michango
na hata rushwa ya ngono kila mara .
“Wakati mwingine
wanatunyanyasa hata kututishia kutunyang’anya mabanda yetu ukizingatia kuwa
tulio wengi tumekodi,” alisema.
Mjasiriamali
mwingine, Mwajuma Rashidi, alisema uongozi huo wa soko umekuwa kero kwao
kutokana na kufanya mambo yao bila kushirikisha wafanyabiashara na haujawahi
kuitisha mkutano hata moja tangu ulipoingia madarakani zaidi ya miaka sita
sasa.
Alisema wamekuwa
wakikabiliawa na changamoto kubwa ya kuombwa rushwa ya ngono kutoka kwa baadhi
ya viongozi na suala hilo liangaliwe kwa makini ili ufumbuzi wake uweze
kupatikana. Alisema kuna wakati dada mmoja aliwahi kuomba kukodishwa banda kwa
ajili ya biashara na akaombwa rushwa ya ngono ambayo aliitoa.
“Kwa bahati mbaya
dada huyo akapata mgonjwa akaenda kumuuguza aliporudi akakuta banda kapewa mtu
mwingine tena anaombwa atoe rushwa ya ngono ili aweze kupatiwa jingine, sasa
tutakua tunatoa ngono kila siku hadi tupate mimba?” alihoji.
Alisema sasa
wamechoka na hawataki tena viongozi hao waendelee kuwa madarakani bali
wachaguliwe wengine.
Kwa upande wake,
Siril Tukia, alisema tangu viongozi hao waingie madarakani miaka sita iliyopita
wamekuwa wakikusanya michango mbalimbali na kuitumia kwa maslahi yao na
wanapotakiwa kuitisha mikutano ya mapato na matumizi wamekuwa wakikwepa.
Mwenyekiti wa soko
hilo, Norbert Pangasero akijibu madai ya wafanyabiashara hao alikiri kuyapokea
malalamiko hayo na kudai kuwa wanatarajia kuitisha mkutano ndani ya wiki hii
ili kusikiliza kero zote.
No comments:
Post a Comment