KATIKA kutatua
changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu nchini, Taasisi ya Econnect
imetengeneza mfumo wa kielektroniki ambao utaisaidia kuimarisha mawasilianio
kati ya utawala wa shule na wazazi au walezi.
Mfumo huo umejikita
katika kutatua changamoto za upatikanaji wa takwimu sahihi na kwa wakati
zinazohusisha idadi ya shule, idadi ya wanafunzi na idadi ya waalimu.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Hashim
Magesa alisema mfumo huo pia utaisaidia serikali kutatua changamoto
zinazolikabili Taifa hasa katika sekta ya elimu ikiwemo kudhibiti tatizo la
utoro.
“Pamoja na tafiti
kuonesha kwamba kuna changamoto za walimu kutofanya kazi ipasavyo na uwepo wa
wanafunzi hewa, pia kuna changamoto ya utoro wa wanafunzi mashuleni ambapo
wanafunzi wanaaga nyumbani wanaenda shuleni lakini hawafiki shuleni na kusubiri
muda wa kurudi nyumbani ndio na wao pia hurudi nyumbani,” alisema.
Pia alisema mfumo
huo utapunguza gharama za uendeshaji zisizo za lazima, kuboresha utendaji wa
kazi kwa walimu kwa ujumla na kusaidia rasilimali fedha na rasilimali watu
kupelekwa sehemu sahihi na kwa wakati sahihi.
Aidha alisema mfumo
huo utasaidia serikali katika kupanga mipango ya maendeleo ya baadaye katika
sekta ya elimu, kusaidia wadau mbalimbali wa elimu kuweza kujua kwa urahisi
mahali shule inapatikana, mandhari yake, mawasiliano yake pamoja na historia
fupi ya shule.
Alisema mfumo huo
pia utawasaidia wadau mbalimbali wa elimu kupata nakala tofauti za vitabu
pamoja na notisi kwa ajili ya kujisomea.
Alisema taasisi hiyo
mara baada ya kukamilisha utengenezaji wa mfumo, iliomba ridhaa kutoka uongozi
wa manispaa ya Ilala ili kukusanya takwimu katika shule zote za awali na msingi
zilizopo ndani ya manispaa hiyo kwa ajili ya kujaribu ufanisi wa mfumo.
“Mara tu baada ya
kupewa ridhaa na uongozi wa Manispaa ya Ilala, Taasisi ya Econnect ilianza kazi
ya ukusanyaji takwimu na kuziingiza kwenye mfumo ambapo jumla ya shule 152
zikiwemo za serikali na za binafsi tulikusanya taarifa zake,” alisema.
Alisema taarifa
walizokusanya ni pamoja na orodha ya wanafunzi kwa majina, jinsia, namba za
simu za wazazi au walezi, idadi ya wanafunzi waliohama na kuhamia, idadi ya
madawati au viti, orodha ya walimu kwa majina, jisnia, masomo anayofundisha,
muda alioanza kazi, daraja lake kwa sasa, kiwango chake cha elimu, namba yake
ya simu pamoja na kumpiga picha.
Taarifa nyingine
walizokusanya katika shule hizo ni idadi ya walimu walihama au kuhamia, idadi
ya walimu waliostaafu, idadi ya walimu walioko masomoni, idadi ya vyumba vya
madarasa vilivyopo, mashimo ya vyoo na idadi ya kompyuta zilizopo, Magesa
alisema serikali itakapouridhia mfumo huo, shule zitaunganishwa bure ila kwa
wazazi watakaopenda kuutumia mfumo huo kwa hiari watachangia sh 300 kwa mwezi.
Hata hivyo,
alipotafutwa, Mkuu wa Wilaya hiyo Sophia Mjema alisema kuwa atafuatilia suala
hilo.
Mkurugenzi wa
Manispaa hiyo, Msongela Valela, aliahidi pia kutoa ufafanuzi leo.
No comments:
Post a Comment