POLISI mkoani Pwani inamshikilia Khalid Mohamed (29) fundi
ujenzi wa Kibaha Kwamathias wilayani Kibaha kwa tuhuma za kuhusika na matukio
mbalimbali ya kihalifu ikiwa ni pamoja na mauaji ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya
Liwale mkoani Lindi Ephrahim Mmbaga.
Mtuhuhumiwa huyo aliyekutwa na bunduki aina ya SMG na risasi 14 ni mmoja wa watuhumiwa 15
waliokiri kuhusika na matukio mbalimbali ikiwemo tukio hilo la mauaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini Kibaha kwa vyombo
vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Bonaventura Mushongi, mtuhumiwa
huyo alikamatwa Machi 2, mwaka saa 11 jioni eneo la Misugusugu Kata ya
Misugusugu Tarafa na Wilaya ya Kibaha.
Mushongi alisema kuwa mtuhumiwa alikamatwa akiwa na silaha
hiyo aina ya SMG ambayo namba zake
zilikuwa zimefutwa pamoja na risasi hizo.
“Mbali ya kukutwa na silaha hiyo pia alikutwa na risasi za
shotgun, mlipuko mmoja, sime moja, mask (kinyago cha kufunika uso) moja na koti
moja vyote vikiwa vimewekwa kwenye mfuko wa rambo ukiwa umefukiwa chini ya
ardhi kwenye shamba la mtu aliyetajwa kwa jina moja la Swai,” alisema Mushongi.
Akielezea juu ya tukio la mauaji ya aliyekuwa Mkuu wa
Wilaya, Kamanda huyo alisema mtuhumiwa huyo na wenzake 15 ambao wanashikiliwa
walikuwa wakijihusisha na matukio mbalimbali mkoani humo likiwemo la kumuua
Mkuu huyo wa Wilaya.
Mkuu huyo wa wilaya ya zamani aliuawa Februari 18, mwaka huu
saa 3:30 usiku eneo la Viziwaziwa tarafa na Wilaya ya Kibaha baada ya
kujeruhiwa na kitu chenye ncha kali ambacho inadhaniwa kuwa ni silaha kwenye
paja la mguu wa kushoto.
No comments:
Post a Comment