RAIS John Magufuli anatarajiwa kuwa
mgeni rasmi katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kitaifa,
huku kilio kikubwa cha vyama vya wafanyakazi kikiwa kukosekana kwa mikataba ya
hali bora kazini.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirikisho
la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Taifa lilipaswa kuwa na
waajiriwa milioni 3.7 katika sekta iliyo rasmi, lakini waliopo ni 650,000
pekee, hali inayoashiria kutokuwa na mikataba.
Katibu Mkuu wa Tucta, Yahaya Msigwa
alisema hayo jana mjini Moshi ikiwa ni maandalizi ya Mei Mosi itakayofanyika
Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU). “Tayari tumemwandikia Rais Dk
Magufuli kumuomba awe mgeni rasmi, kimsingi sherehe zote kitaifa mgeni rasmi ni
yeye...tunazo ajenda za kumpa Rais, lakini moja ya mambo ambayo ni kero ni hili
la mikataba ya hali bora kazini, wafanyakazi wengi wanafanya kazi kama vibarua
na hawajui haki zao,” alieleza Msigwa.
Alitolea mfano wa watumishi wa
mashambani pekee nchini Kenya ni zaidi ya 700,000 na Afrika Kusini ni zaidi ya
milioni moja na kwamba ipo haja kwa waajiri Tanzania kutafakari upya suala la
maslahi ya wafanyakazi wao na rais anapaswa kulisemea hilo.
Aidha, Katibu Mkuu huyo wa Tucta
alitaka waajiri kuruhusu kuundwa kwa mabaraza ya wafanyakazi sehemu za kazi ili
kutoa fursa kwa wafanyakazi kukutana na kujadili maslahi yao lakini pia kufanya
kazi kwa tija zaidi.
Katika hatua nyingine, Msigwa alisema
Tucta inaunga mkono kampeni ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kupambana na
wafanyakazi hewa sanjari na mpango wa kupunguza matumizi ya serikali.
“Pamoja na nia njema ya serikali
katika kupambana na wafanyakazi hewa, lakini tunaomba haki itendeke na isitokee
mfanyakazi ameonewa kwa namna yoyote ile kwani huko ni kuwakatisha tamaa
wafanyakazi waadilifu na waaminifu,” alieleza. Maadhimisho ya Mei Mosi
yatahusisha pia kujengwa kwa mabanda ya kuoneshwa kwa shughuli mbalimbali za
kisekta nchini.
No comments:
Post a Comment