RAIS
John Magufuli amewafuta kazi watumishi 9,932 wa serikali waliobainika kuwa na
vyeti feki na kuagiza kusitishwa mara moja mishahara yao, huku akiwataka
waondoke kazini mara moja na watakaokaidi agizo hilo watashitakiwa mahakamani.
Pia
ameagiza majina ya watumishi hao yatangazwe kwenye magazeti ili watu waone na
wajifunze kuwa waliiibia serikali fedha kwa kukaa kwenye nafasi ambazo si zao.
Kwa mujibu wa sheria, mtumishi aliyeghushi cheti anakabiliwa na kifungo cha
miaka saba gerezani.
Rais
Magufuli alisema hayo jana mjini hapa baada ya kupokea taarifa ya uhakiki wa
vyeti kwa watumishi wa umma sambamba na uzinduzi wa sherehe za miaka 10 tangu
kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Rais
Magufuli alisema ni lazima watumishi hao waondoke kwenye utumishi wa umma mara
moja kutokana na kuisababishia serikali hasara kubwa. “Tena naagiza mshahara
wao wa mwezi huu ukatwe na waondoke kwenye utumishi wa umma, watakaokaidi
watapelekwa mahakamani kwa mujibu wa sheria na nafasi hizo 9,932 zitangazwe ili
wasomi waweze kuziomba.
Hao ni
majambazi na wezi kama walivyo wezi wengine, hatukusema mtu kuwa na sifa ya
kuajiriwa mpaka uwe na digrii lakini haiwezekani kushikilia nafasi ambayo si
yako, kama umeshindwa kufikia sehemu fulani usiruke nenda kwenye elimu ya
kujiendeleza utafika lakini usidanganye.
Hili
ni fundisho kwa watu waliozoea kughushi, mkafute majina yao yote kwenye
kompyuta, orodha ninayo waondoke wenyewe kwa hiyari kabla ya kupelekwa
mahakamani.”
Aliwataka
wakatafute kazi ambazo zinalingana na elimu zao. Alisema mpaka Mei 15, mwaka
huu watumishi wote walioghushi vyeti wawe wameondoka kwenye utumishi wa umma na
wasipoondoka vyombo vya dola wawachukulie hatua, wapelekwe mahakamani wakajibu
vyeti vyao wamechapisha wapi.
Aidha
alitaka watumishi 1,538 ambao vyeti vyao vina utata mpaka Mei 15, mwaka huu,
hatma yao ijulikane na kama wanajijua kuwa si wahusika wa vyeti hivyo waondoke
mapema.
“Hapo
tutakuwa tumetengeneza ajira 12,000, si haba kwa wasomi, “ alisema. Pia alitaka
waliowasilisha vyeti vya utaalamu bila kuwa na vyeti vingine wafuatiliwe. “Kuna
wengine wamejiendeleza hatua kwa hatua si lazima wafike kidato cha sita,
watumishi hao 11,566 waendelee kulipwa mishahara yao ila uchunguzi ufanyike,”
alisema.
Alisema
tayari serikali imetangaza nafasi za ajira 52,456 ukiongeza na nafasi 12,000 za
watumishi wenye vyeti bandia na vyenye utata, Watanzania wengi wenye sifa
wataajiriwa serikalini.
“Hatua
nyingi tunazochukua si za kumkomoa mtu, kila mmoja analalamika, tunataka
kuipeleka Tanzania mahali fulani tunaomba ‘sapoti’ ya Watanzania, tunafanya
yale yenye manufaa kwa Watanzania.
Hatutaki
kulaumu watu waliopita ila tukumbuke dhambi walizofanya tusiporekebisha
tutaendelea na mfumo huo huo. Kwani hawakuwepo mawaziri, wakurugenzi ila makosa
waliyofanya sisi tuone wana nafasi ya kurekebisha,” alisema.
Rais
Magufuli alisema serikali imejipanga kufanya kazi hasa kwa ajili ya Watanzania
wanyonge na taifa hili ni tajiri. Alisema mapato ya serikali yanayokusanywa
yameongezeka ambapo awali makusanyo ya mwezi yalikuwa ni Sh bilioni 800 ambayo
sasa yamefikia Sh bilioni 850 na fedha za kulipa mishahara zilikuwa ni Sh
bilioni 700.
“Huwezi
kuendesha nchi kwa Sh bilioni 100 na kumbe fedha nyingi zilikuwa zikienda
kulipa watumishi hewa, sasa tunavuna Sh trilioni 1.3 na hatujafanikiwa sana,
bado kuna maeneo mengi fedha zinaibwa,” alisema.
Rais
Magufuli alisema serikali ilifanikiwa kuwaondoa watumishi hewa serikalini
19,706 ambao walikuwa wakilipwa Sh bilioni 19.8 kwa mwezi na kwa mwaka walikuwa
wakilipwa Sh bilioni 238. Alisema serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwenye
elimu kuanzia ya msingi hadi vyuo vikuu.
Alisema
jumla ya Sh bilioni 483 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya
juu 124,711 kutoka wanafunzi 98,320 waliokuwa wakipata mikopo mwaka jana. Kwa
upande wake Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema wenye vyeti visivyo halali
lazima waondoke kwenye utumishi wa umma kwani wanapoteza nafasi za watu ambao
wana sifa za kuajiriwa kwenye nafasi hizo.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Angellah Kairuki alisema; “ Uhakiki huu haujafanyika kwa viongozi wa kisiasa
ambao wako serikalini kama vile Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao
mamlaka ya uteuzi ndio wanajua ufanisi wa kazi zao na pia katika siasa suala ni
kujua kusoma na kuandika.” Waziri alisema watumishi wa umma wataajiriwa
kulingana na sifa zilizoainishwa kwenye miongozo mbalimbali.
Alisema
uhakiki wa vyeti uliofanyika ni wa kidato cha nne na sita na vyeti vya ualimu
na diploma. Alisema uhakiki huo ulifanyika kwa watumishi wa serikali za mitaa,
mashirika ya umma, wakala wa serikali, serikali kuu, wizara na idara
zinazojitegemea.
Alisema
kati ya vyeti 1,114 vilivyowasilishwa Baraza la Mitihani kwa uhakiki, vyeti 344
vilikuwa vikifanana na watumishi hao walichukuliwa hatua kwa kufikishwa kwenye
vyombo vya sheria.
Alisema
matokeo ya uhakiki kundi la kwanza watumishi 376,969 sawa na asilimia 94.3
walikuwa na vyeti halali na Baraza la Mitihani limejiridhisha magamba ya vyeti
yaliyohakikiwa yalitolewa na baraza hilo.
Alisema
watumishi 9,932 sawa na asilimia 2.4 walibainika kuwa na vyeti vya kughushi
kutokana na miundo ya vyeti vyao kutofanana na vyeti husika. Pia watumishi
wenye vyeti vyenye utata vilivyohakikiwa ni 1,538 sawa na asilimia 0.3.
Waziri
huyo alisema watumishi 11,566 sawa na asilimia 2.8 waliwasilisha vyeti vya
utaalamu peke yake bila cheti cha kidato cha nne au cha sita na wanafuatilia
kwa makini ili kujua mwisho wake. “Suala la kughushi ni kosa la jinai na hatua
zitachukuliwa kwa mawakala wanaotengeneza vyeti vya kughushi.”
Alisema
katika sheria za nchi adhabu za mtu anayeghushi cheti ni kifungo cha miaka
mitano gerezani. Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi,
Profesa Joyce Ndalichako alisema kumekuwa na changamoto kubwa ya kughushi vyeti
vya taaluma au kutumia vyeti vya watu wengine.
Alisema
mwaka 2008 ulianzishwa utaratibu wa kuweka picha kwenye vyeti na kuliongezeka
maficho yanayowekwa kwenye vyeti vinavyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa.
No comments:
Post a Comment