Wakati malalamiko ya changamoto zinazotokana na matumizi ya mitandao ya kijamii zikizidi kuongezeka hasa katika mmomonyoko wa maadili bado kuna fursa nyingi sana katika mitandao hii ambazo hazitumiki ipasavyo.
Jamii hasa vijana wamekuwa wakitumia vibaya teknolojia hii kiasi cha serikali na taasisi mbali mbali kutengeneza taratibu na sheria za kudhibiti matumizi yake ili yasilete madhara makubwa kwa watumiaji au watu wengine wanaoweza kuathirika na matumizi ya watumiaji hao.
Jamii hasa vijana wamekuwa wakitumia vibaya teknolojia hii kiasi cha serikali na taasisi mbali mbali kutengeneza taratibu na sheria za kudhibiti matumizi yake ili yasilete madhara makubwa kwa watumiaji au watu wengine wanaoweza kuathirika na matumizi ya watumiaji hao.
Hebu tuanze na maswali machache kwa wewe unaye soma makala haya; upo kwenye mitandao mingapi ya kijamii? Katika hiyo mitandao upo kwenye makundi (ma-group) mangapi? Je, yana msaada gani kwako?
Hivi karibuni nilijikuta kwenye kundi la mtandao wa kijamii la WhatsApp kwa kuunganishwa na mtu mwingine bila ridhaa yangu. Nikamuuliza maswali machache tu; kwa nini umeniweka kwenye kundi hili na malengo ya kikundi ni nini? Alinipa jibu moja tu kuwa, ‘just for fun’ akimaanisha ni la kujifurahisha. Makundi mengi ya aina hii ni mengi sana kwenye mitandao ya kijamii. Yanatupotezea muda, yanatungizia gharama, yanasababisha uvivu na mara nyingi kuchangia katika mmomonyoko wa maadili kwa sababu ya taarifa, picha na video zinazotumwa kwenye ma-group haya.
Ni fursa zipi tunazoweza kuzitumia katika mitandao ya kijamii na kutusaidia katika kutengeza ajira na kuongeza kipato?
Kutengeneza vikundi vya uzalishaji mali
Kukua kwa tatizo la ajira kuna hitaji mbinu mbadala za kukabiliana nazo ili kujikwamua kiuchumi. Utengenezaji wa vikundi ni moja ya njia rahisi za kukabiliana na tatizo hili. Changamoto kubwa ya kuunda vikundi hivi ni umbali wa kijiografia kati ya mtu na mtu lakini pia ni ufinyu wa muda wa kukutana mara kwa mara kwa ajili ya mipango na mikakati ya vikundi. Mitandao ya kijamii inatoa fursa kuunda vikundi ndnai ya mitandao hiyo kuwawezesha watumiaji kujadiliana popote walipo.
Kimaro ni mwenyekiti wa kikundi kinachoitwa Afrotan. Kikundi kilianzishwa kwa malengo ya kufanya shughuli za kilimo na ufugaji. Kwa sababu ya changamoto ya muda na umbali aliwashirikisha baadhi ya marafiki na kuamua kutengeza kundi kwenye mtandao wa WhatsApp ambalo hutumika kwa ajili ya majadiliano juu ya mustakabali wa kikundi. Wakati kikundi kinaanza wanachama walikubalina kuwe gharama za kiingilio na michango ya mwezi kwa kuanza na wanachama sita mwaka 2016 na sasa lina wanachama kumi na tano. Kikundi kilianza na mradi wa kulima vitungu na kufuga sungura kwa kuajiri watu na wanachama kushiriki pale wanapopata muda. Baadae wanachama walikubalina kutumia mtaji ulipo kwa ajili ya kukopeshana kwa riba ndogo ili kukuza mfuko na kuwawezesha wanachama kufanya shughuli mbali mbali ikiwemo ujasiriamali. Mpaka sasa kikundi kimeshatoa mikopo ya zaidi ya shilingi 14,000,000/- kwa wanachama.
Hii imewezeshwa kwa kiasi kikubwa sana na uwepo wa kundi la WhatsApp kwani wanachama wapo mikoa tofauti tofauti. Kitu kama hiki kinaweza kufanywa na watu wengi sana na pengine kubadili matumizi ya makundi yaliyopo kwenye mitandao ya kijamii ili kuleta tija zaidi.
Hebu jiulize tena makundi yako yanakusaidia nini?
Biashara na masoko
Kwa kuzingatia kuwa watumiaji wa mitandao ya kijamii ni wengi sana hii inatoa fursa kwa watu wanaoamua kutangaza biashara zao. Watu hutumia akaunti zao za mitandao ya kijamii katika kutoa taarifa juu ya bidhaa na huduma wanazotoa ili kuwajulisha wateja wao kama njia ya kutafuta masoko ya biashara zao. Urahisi na gharama ndogo sana ya kutangaza biashara yako hufanya matumizi ya mitandao ya kijamii kuwa ya ufanisi sana kufikia watu wengi sana ambao wanauwezo wa kuwasilina nawe moja kwa moja kupitia mitandao hiyo hiyo ya kijamii. Utafutaji wa masoko hufanyika pia kwenye makundi yanayotengenezwa kwenye mitandao hiyo.
Elimu ya ujasirimali
Mitandao ya kijamii inatoa fursa ya kutoa elimu na taarifa zinawezeka kusaidia katika ujasirimali na kutengeneza ajira kwa wengine. Elimu ya ujasirimali imekuwa ikifanyika kwenye mitandao ya kijamii kwa baadhi ya watu ambao wameshaiona fursa hii. Watu wenye maarifa au uzoefu wa biashara wamekuwa wakifundisha wengine kupitia kurasa zao na makundi yanayo undwa kwenye mitandao ya kijamii. Shughuli hii hufanyika bure na wakati mwingine kwa kiasi fulani cha ada. Sasa kama una ujuzi na unaweza kutumia ujuzi wako kwa kufundisha wengine usitafute kisingizio kuwa hauna fedha za kukodisha darasa au ukumbi, waweza toa elimu kupitia mitandao ya kijamii. Pia, mtandao kama YouTube una mamilioni ya video zinafundisha mambo mengi sana ikiwemo biashara na ujasirimali. Video hizi zinaweza kukupa maarifa zaidi na kukuhamasisha kuanza au kukuza biashara yako na hakuna malipo unayoyafanya kwa kuangalia.
Fursa za ajira
Kuwa na elimu ya matumizi ya mitandao ya kijamii kunatoa fursa kwa vijana wengi. Wapo wanaofahamu nguvu ya mitandao ya kijamii katika kutafuta masoko lakini hawana ujuzi wa kutumia mitandao hii. Hawa hugeuka fursa kwa wale wenye ujuzi wa kutosha kwani huwalipa wenye ujuzi ili wawatengenezee na kuzisimamia kurasa za mitandao ya kijamii. Shughuli hii mara nyingi haifanywi bure bali kwa malipo kutokana na makubaliano yanayofikiwa. Kama haujui, taasisi mbali mbali na watu wengi maarufu uwa hanawana muda kusimamia kurasa zao kwenye hiyo mitandao ya kijamii lakini huwa na wasaidizi katika shughuli hiyo.
Pamoja na hilo, zipo kurasa za mitandao ya kijamii zenye wafuasi wengi sana kiasi cha watu binafsi na makumpuni kuwalipa wenye kurasa hizo ili wawatangazie biashara zao. hii ni fursa pia ya kujipatia kipato kwa sababu shughuli hii huwa haifanywi bure pia.
Angalizo
Mitandao ya kijamii pia imewacha madhara mengi katika mahusino ya kibiashara kwani wapo wanaotapeliwa na kupoteza fedha zao. hivyo ni vyema kuwa muangalifu unapo amua kuanzisha mahusiano yoyote ya kibiashara kupitia mitandao ya kijamii. Kama unataka kuanzisha kikundi cha biashara kwenye mitandao ya kijamii zingatia kuwa na wanachama mnaofahamiana na kuaminiana pia.
(Makala haya yalichapishwa kwenye gazeti la Mwananchi tarehe 11 Novemba, 2017)
No comments:
Post a Comment