Monday, 27 November 2017
Siri ya Kuongeza Kipato Ukiwa Bado Kijana
Kila siku tunalala na kuamka, kama kawaida ya binadamu, tumekuwa tukibadilika siku hata siku.
Mabadiliko haya yanahusisha kubadilika mwili na mwonekano tena zaidi ni kuongeza miaka iliyoishi duniani.
Ukiwauliza matajiri wote duniani, wanakwambia kuwa ili uweze kuwa na kipato kikubwa katika familia hakikisha unawekeza ukiwa bado na umri mdogo, hasa katika umri wa miaka 20 hadi 45. Wachumi wanasema ni rahisi sana kutengeneza kipato katika umri huu kwa sababu ni wakati ambao binadamu anakuwa na nguvu za kutosha, akili pia inakuwa juu zaidi katika kufikiri na kupanga mipango mbali mbali kuliko umri wa uzee ambao mara nyingi mwanadamu huanza kurudi katika hali ya utoto.
Katika jamii yetu wazee kuanzia miaka 50 na kuendelea ndiyo wanahangaika na kutafuta pesa kwa ajili ya kuongeza kipato cha familia, lakini wenye umri wa ujana wao ni kinyume chake. Wao wanahangaika na kutafuta wanawake tena mbaya zaidi siyo wa kuoa bali wa kufurahia nao tu tendo la ndoa na kuondoka. Hili linajumuisha zaidi hasa ukibahatika kusikiliza mazungumzo yao katika vijiwe.
Unayesoma makala haya, kama wewe ni kijana wa umri wa miaka kuanzia 20 hadi 45, anza kuwekeza katika umri huu, ziko njia mbali mbali zitakazo kusaidia kuwekeza.
Wengi wetu tunaogopa benki, ninaposema kwenda benki sina maana ya kwenda kukopa pesa ingawa pia inaweza kuwa hivyo ila mimi nazungumzia namna wafanyakazi wa benki watakavyoweza kukusaidia wazo la kukusaidia wewe katika uwekezaji wako.
Nenda benki katika kitengo cha biashara na uchumi, nadhani kila benki kitengo hiki kipo. Kazi yake kubwa pamoja na mambo mengine ya kibenki, kinatoa msaada wa elimu kwa wajasiliamali na wafanyabiashara wakubwa kwa namna gani wakeze biashara zao. Ukienda pale ukajitamburisha kuwa unataka uanze biashara au uwekezaji wako watakushauri vizuri sana.
Lakini pia kama unapata pesa kidogo mwisho wa mwezi, tumia hicho hicho kiasi kufanya uwekezaji, kwa mtu yeyote ambaye ana nia ya dhati katika uwekezaji, kila pesa anayoipata hata kama ni ndogo kivipi, lazima atenge kidogo ili aifanikishe maana hilo ndilo litakalomfanya aishi kifahari.
Watu wengi wamekuwa wakijihusisha na mambo ambayo hayana tija katika kuinua uchumi wao katika familia, hii yote ni kutokana na kuiga iga mambo katika mitaa, ambayo kwa kiasi kikubwa yameshapitwa na wakati.
Kusoma kuongeza elimu ni vizuri, na hata sasa wapo ambao wamefikia hadi PhD lakini bado kipato chao kinalegalega, hii ni kwa sababu mtu atambui kuwa kama tayari una fani, iwe diploma, hadi digrii tayari wewe ni msomi, ukitaka kuongeza digrii nyingine maana yake unatafuta kitu kinaitwa "Value added" lakini mambo ni yaleyale. Astashahada au stashahada zinatosha kabisa kumkomboa mtu kupitia hiyo elimu.
Endelea na wewe kuchunguza kwa umakini, ile orodha ya matajiri duniani kuna mtu aliye na vyeo hivi? Dr, Profesa, ? Ukienda kufanya uwekezaji kwa kujigamba kuwa wewe una digrii tatu, Masters, mara oooh Profesa ujue kabisa unajiandaa kushindwa kuendelea katika hiyo biashara.
Changamka wakati ndiyo huu, unisubiri kesho. Baada ya miaka 10 ijayo wewe utakuwa na miaka mingapi? Je, una ndoto za kuwa na familia? Je, unawaza nini kuhusu namna watakavyoishi na wewe wakati hukujiandaa wakati wa ujana? Unajisikiaje kuiacha familia na kukimbilia kusikojulikana kwa kushindwa kuisimamia familia yako? Amua sasa, anza sasa achana na mambo ya ajabu yasiyo na faida katika maisha yako.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment