Habari motomoto zilizojili hivi punde kutoka kila kona ya Dunia

Sunday, 26 November 2017

Unataka Kuwa Mjasiliamali? Chukua Mbinu Hizi!




Mtu anaweza kujiuliza atawezaje kuwa na mtazamo chanya wakati mambo hayaendi sawa katika biashara.


Zifuatazo ni baadhi ya mbinu  ambazo wajasiriamali wanaweza kuzitumia ili kujijengea uwezo wa kuwa na mtazamo chanya ili kuweza kujenga mafanikio.

Mbinu ya kwanza ni kujiamini. Jiamini, jiamini, jiamini unaweza na kwamba una mengi ndani yako kuweza kuyafanya ili kupata mafanikio unayotamani. Ni vizuri kuamini juu ya uwezo ulio nao katika kujitafutia mafanikio badala ya kufikiria namna ya kukabiliana na mapungufu yako.
Utakuta mjasiriamali hajiamini, anakosa hata uwezo wa kusimama mahali na kuwashawishi watu juu ya bidhaa fulani anayotengeneza mwenyewe na kwa hali hii kukosa fursa mbalimbali za kibiashara. Kumbuka jinsi utakavyoweza kujiamini ndivyo utakavyoweza kujiongezea fursa.
Wajasiriamali wengi hujiangalia kwa vile vitu ambavyo hawana na kuangalia wenzao wana nini! Wakati wote sahau kuangalia juu ya nini wewe hauna na elekeza akili yako kwa kile ulichonacho, hata kama ni kidogo. Kwa kuwa nacho hicho kidogo uwe mwanzo wa kutafuta fursa zaidi.
Mbinu ya pili, kuwa na wigo wa marafiki wenye kufaa katika biashara yako. Usitegemee kupata mafanikio kama umezungukwa na watu wenye mtazamo hasi. Watu wenye mtazamo hasi watakukwamisha, watakukatisha tamaa, epukana na wale watu wasemao si tulikwambia!
Je kati ya marafiki zako ulio nao katika biashara ni wangapi hukutia moyo pindi mambo yanapokuwa si mazuri?  Je una mtu unayemuamini kumwambia magumu yanayokusonga katika kile unachofanya? Haya yote unaweza kuyafanya kwa kuwa na watu wenye kufaa.
Unahitaji kuwa na mtandao wa marafiki katika biashara wenye kukusaidia, unahitaji kuwa na muda wa kuhudhuria shughuli maalum za kijamii. Kumbuka unapokuwa katika mtandao wenye kufaa katika biashara ndivyo utakavyo weza kujifunza na kujijengea mtazamo chanya.
Ni muhimu kuelewa na kukubali kuwa si kila mtu hata ndugu zako wanaweza kufurahia mafanikio yako, kuelewa hili litakusaidia kukupa nguvu na kusonga mbele. Kwa kuwa hufanyi mambo kwa kumfurahisha mtu, ni vizuri kuwa mtu wa kusoma alama za nyakati!
Mbinu ya tatu ni kutafuta watu wa kujifunza toka kwao (role models). Wakati unapopitia kipindi kigumu katika biashara zako kumbuka kwamba hauko peke yako. Kumbuka magumu katika safari za kibiashara hayatokei kwako peke yako na wewe sio wa kwanza.
Kumbuka kwamba, magumu yametokea kabla kwa watu mbalimbali na yatatokea tena. Ambacho unatakiwa kukifanya ni kujifunza kutokana na yaliyotokea na kuyaona ili kuweza kusonga mbele. Hivyo magumu unayoyaona toka kwa wengine yawe pia fursa ya wewe kujifunza.
Mtafute mjasiriamali yoyote unayeona amefanikiwa na umuulize kuhusu safari yake ya mafanikio, anaweza kuwa shuhuda mzuri wa namna ya kukabiliana na magumu katika maisha ya kila siku. Mafanikio sio suala la kulala na kuamka kumbuka safari ni hatua!
Mbinu ya nne ni kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Unaweza wakati mwingine ukafikiri kwamba mafanikio katika biashara zako yanatokana na bidii zako mwenyewe, yafaa kukumbuka kuwa bidii na uelewa wako si peke yake vyenye nguvu za kukuletea mafanikio.
Wajasiriamali yawapasa wakumbuke kuwa wote wana deni kwa Mwenyezi Mungu kwa mafanikio yote wanayoyapata. Hata wakati unapokumbana na magumu yapasa kuchukulia kama changamoto katika imani uliyonayo na hii itakuwezesha kuwa na mtazamo chanya.
Mbinu ya tano pamoja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu yafaa kujifunza kuwa mtu wa kutoa. Badala ya wakati wote kujifikiria wewe mwenyewe na familia yako, yafaa kujijengea utamaduni wa kuwasaidia wengine hasa wasio na uwezo.
Vitabu vyote vya dini vinasisitiza kwa waamini wao kuwa na moyo wa kuwasaidia wengine ambao hawakuweza kujaliwa. Sasa ni wakati muafaka hasa tunapoelekea mwisho wa mwaka kuangalia yale tuliyofanikiwa na kuweza kuwasaidia wengine wanaohitaji.
Tafuta namna ya kuwasaidia wengine kama njia ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa jinsi ambavyo amekuwezesha .Kwa njia hii utakuwa umejijengea mtazamo chanya na hasa kwa kujua kwamba umeweza kugusa maisha ya wengine kwa msaada wako.
Mbinu ya sita kuwa na ndoto kubwa ya kusisimua, unaweza kujiuliza ndoto kubwa ya kusisimua ni ipi. Katika kufikiria hili yafaa kujifunza toka kwa baadhi ya waliofanikiwa akiwemo Rais Barrack Obama wa Marekani.
Ukisoma historia ya Obama na kama ulifuatilia kampeni zake tangu muhula wa kwanza mpaka alivyoweza kutetea tena kiti chake cha urais utagundua nguvu iliyopo katika kuwa na ndoto  kubwa ambazo zitaweza kukusisimua katika kuzitafutia mafanikio ili ziwe kweli.
Huo ni moja ya mifano ya kufikia ndoto kubwa, tatizo kubwa lililopo miongoni mwa wajasiriamali ni ile hali ya kuwa na ndoto ndogo za kawaida. Kununua gari, kujenga nyumba, kuwa na uwezo wa kumsomesha mtoto katika shule za ‘academy’ nakadhalika.
Kuwa na ndoto kubwa katika ujasiriamali kutakusaidia kuwa na mtazamo chanya kwenye mihangahiko unayofanya kufikia ndoto hizo. Wakati utakapokaa chini ili kuweza kujiwekea malengo kwa mwaka mpya ujao, jaribu kuwa na ndoto kubwa zikusukume kufikia makubwa.
Mbinu nyingine unayoweza kuitumia ili kujijengea mtazamo chanya ni kuwa mtu wa kushukuru. Mshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukufikisha hapo ulipo bila kujali umefanikiwa kiasi gani, yafaa kuwa na shukrani kwa wafanyakazi wako, familia na wote walioweza kukusaidia.
Vilevile yakupasa kutojilaumu mwenyewe au kuwalaumu wengine kama mambo hayakwenda vizuri, wasamehe wote waliokukwaza hapa na pale.
MAKALA HAYA YALIANDIKWA KWENYE GAZETI LA NIPASHE SEPTEMBA 30, 2016 NAMI NIKAONA TUSAIDIANE HII ELIMU ILI TUFIKE MBALI KIUCHUMI

No comments:

Post a Comment