AWALI ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kutulinda, kutupa uhai na afya njema hadi leo. Yote yamewezekana kwa kuwa
amependa sisi wajoli wake tuwe hai na wenye afya.
Wako wenzetu wakati
huu wako hospitali au vitandani
kutokana na maradhi mbalimbali. Tuwaombee wote walio wagonjwa.
Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kujua kwanini wengine kawapa
afya njema na wengine kawapa maradhi ya aina mbalimbali. Inawezekana kati ya
mnaosoma makala hii sasa, wengine hamtaweza kuuona mwaka 2018.
Ndugu zangu Watanzania, ili tuweze kuwa na
matumaini ya mwaka mpya wa 2017 tuliouanza, ni vema takatafakari mwaka
tunaouaga wa 2016.
Huu ni mwaka wa kwanza tangu Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015,
ambapo tulimpata Rais mpya, John Magufuli na kuunda serikali yake. Ni
dhahiri kila tunapoingia kwenye uchaguzi, kila mmoja wetu huwa na matumaini ya
matokeo ya uchaguzi kuleta unafuu katika maisha yetu ya kila siku.
Ndio maana wakati wa kampeni, tunasikiliza kwa umakini
sera mbalimbali zinazoletwa kwetu. Hatimaye tunapiga
kura kuichagua ile sera ambayo kila mmoja kwenye nafsi yake anaamini itamletea
unafuu, itamtoa pale alipo kuelekea kwenye maisha bora.
Kwa wengine ni matumaini ya kutoka kwenye maumivu ya maisha
kwenda kwenye unafuu. Kwa uzoefu wangu
wa ubunge wa miaka
15 na miaka 20
kwenye siasa ( active
politics), ninaelewa kabisa kuwa wako ambao siku ya pili
baada ya uchaguzi wanataka kuona kero zao
zimeondoka.
Kama tatizo lilikuwa
maji safi na salama, hawaelewi,
baada ya kumpata kiongozi kwanini siku ya pili, ya tatu, mwezi na hata mwaka
baadaye hakuna maji!
Hii ni hali ya kawaida kwa binadamu. Mimi
nilichaguliwa na watu wa Karatu
kutokana na kero kubwa ya
maji wilayani Karatu. Maji yalidhalilisha utu wa binadamu hasa akinamama.
Maji yalifanya watoto wadogo kubakwa kwenye vituo
vichache vya maji
vilivyokuwepo. Maji yalifanya mahudhurio
ya watoto shule za msingi yadorore
kwa kuwa watoto walikesha usiku kucha kusubiri
maji kwenye vituo vichache vya maji.
Nakumbuka kila nikipita mitaani, nilianza
kuitwa tapeli kwa kuwa
miezi sita baadaye, na kisha mwaka
mmoja baadaye, maji yalikuwa
hayajaonekana kwao. Mwananchi
wa kawaida yeye hajui jitihada
unazofanya kuleta maji.
Yeye kazi yake ilikuwa kupiga kura, mengine hayamhusu. Hajui
kuwa maadui zako wanakuhujumu na kukuvuta chini ili usifanikiwe, kwani
kufanikiwa kwako ni kuonyesha udhaifu wao.
Mwananchi haelewi kuwa mikakati ya utekelezaji wa
mradi wowote haina budi kuandaliwa kwa
umakini, fedha zitafutwe, kazi ya usanifu
lazima ifanyike.
Kwa Karatu, maji
yalianza kutoka kwenye mabomba mwaka 2000, wakati
uchaguzi ulikuwa 1995. Tone
la kwanza la maji lilipotoka,
wananchi hata waliokata tamaa, waliodhani wametapeliwa walilipuka
kwa furaha ya ajabu.
Walisahau matusi yote waliyokuwa wamenishushia. Sasa
wakaanza kubaini kwamba kumbe hawakuwa wakidanganywa. Waliokuwa
wavumilivu waliona na
kushuhudia hatua zote za
utekelezaji wa mradi.
Waliokuwa wepesi kukata tamaa nusura watukatishe tamaa sisi
watekelezaji kwa kejeli, kebehi, matusi tuliyokuwa tukimwagiwa mitaani.
Uvumilivu ulizaa matunda. Wananchi takribani 30,000 walipata
maji ya uhakika ndani ya nyumba zao, wengine katikati ya kitongoji chao,
vitongoji vingine vilikuwa na DP ( Distribution Points) zaidi ya mbili au tatu.
Hivyo mama anaenda na sufuria na akirudi anabandika jikoni.
Hili ni tunda la uvumilivu. Ndugu zangu
nimeeleza kidogo kwa kirefu
hadithi hii ambayo ilinipata
mimi na wananchi wangu wa
Karatu.
Ninafahamu pia kwamba mara baada ya ushindi wa Magufuli,
makundi tofauti ya wananchi yatakuwa na matumaini tofauti kuhusu matarajio ya nini
watakachokipata.
Wamachinga walijua
mikopo midogo midogo itapatikana kwa
urahisi, na hawatakimbizwa tena mitaani
kama mbwa. Bodaboda waliozuiliwa kuingia katikati ya miji walijua
sasa wamefunguliwa milango na hivyo biashara yao itakuwa rahisi.
Hali hii iko hivyo kwa takribani makundi yote ya kijamii.
Kwa miaka mingi, wananchi wetu wameaminishwa kuwa nchi yetu ni tajiri na hivyo
wana matarajio makubwa kwa viongozi wao.
Tuna rasilimali za kila aina kuanzia rasilimali chini ya
bahari na maziwa yetu, magogo kwenye misitu yetu, rasilimali wanyamapori, ikiwa
ni pamoja na “twiga wetu” aliyekunjwa shingo na kuingizwa kwenye
ndege kutoroshwa.
Kuna kero nyingine pia kama vile maelfu ya tembo
na faru waliokuwa wakiuawa
bila huruma na majangili
kwa manufaa yao binafsi, fedha zetu kwenye benki
kuibiwa hovyo nakadhalika.
Wananchi haohao wamesahau kuwa mara baada ya uchaguzi, kazi
kubwa ni mapambano dhidi ya “ wahujumu hao”. Kwa
bahati mbaya “mpira
usiocheza hujui si rahisi
kujua ugumu wake. Kumbe hata
ukiachiwa peke yako ufunge bao kwenye goli lililo wazi, unaweza kuupaisha juu
kwa mshangao wa wengi!”
Hivi ndivyo ilivyo kwa serikali. Natambua kabisa
watumishi wa umma walitegemea mishahara itapanda na
kukidhi mahitaji yao, wanafunzi wa vyuo walijua mikopo sasa itakuwa
rahisi na itatoka kwa wakati.
Wazazi walijua “ elimu itakuwa bure hadi kidato cha nne” na
hawatasumbuliwa tena, hata kero ya madawati itatatuliwa bila mwananchi kuguswa
kabisa! Natambua kuwa matamanio hayo si tu hayakutekelezwa bali maumivu
yalikuwa makubwa zaidi kwa mwaka wote
wa 2016.
Mitaji imepotea,
mabenki hayakukopesha kwa hofu
mbalimbali, mzunguko wa fedha ulikauka, hata wenye mitaji yao midogo ikaliwa. Hoteli
nyingi kufungwa kwa kushindwa
kulipa mikopo kutokana na
kutokupata wateja.
Watumishi wa umma hawakupewa mishahara iliyotangazwa
kupanda. Hii ni hali ngumu na ninatoa pole sana kwa wale wote, kwa makundi yao,
walioumia kwa namna moja au nyingine.
Kazi ya kwanza
ya kiongozi yeyote makini
anaposhika dola ni
kuangalia mianya mbalimbali ya wizi na uozo wowote katika
usimamizi wa rasilimali za umma. Nadhani wote tunakiri serikali hii ilipoingia
tu madarakani, jambo la kwanza lilikuwa kubaini wafanyakazi hewa.
Leo tunazungumzia wafanyakazi hewa
takribani 20,000. Fikiria ni mabilioni
mangapi kwa mwezi yalienda
kwa wafanyakazi hewa? Ni
dhahiri fedha hizi zingelitengeneza
mzunguko wa fedha kama
zingelikuwa kwenye mkondo sahihi.
Hakuna shaka kwenye hilo.
Lakini ni wafanyikazi
hewa, hivyo taifa halikuzalisha
kutokana na wafanyakazi hao
hewa. Ghafla uhakiki unaonyesha kuwa kuna siyo tu waalimu hewa, lakini
wanafunzi hewa zaidi ya 60,000.
Mungu atusamehe!
Sijui tumelogwa! Taifa
la ajabu. Watu “wanatumbua” bila aibu. Hawa
walikuwa wakitumbua fedha zetu kwa manufaa ya “ matumbo yao” na familia
zao.
Hatujakaa sawa tukaambiwa kuwa hata fedha za TASAF
zilizolenga kusaidia kaya
maskini sana nazo zimeliwa.
Kaya takribani 55,000 zilizokuwa zinufaike
zimekosa huku baadhi ya viongozi
wa serikali wa ngazi mbalimbali, wakiwemo
maofisa wa TASAF wenyewe wakidaiwa kuhusika na wizi huo.
Hatujatulia mara maelfu ya wanafunzi ambao hawakuwa na sifa
za kujiunga na elimu ya Chuo Kikuu walipewa nafasi! Ni dhahiri kuwa
wazazi wa watoto waliofukuzwa wameumizwa na hatua hii.
Lakini ipi nafuu kuendelea kuwa nao na kuathiri ubora wa
elimu hasa katika dunia ya leo ya ushindani. Wenzetu kila siku
wanapambana na ugunduzi wa mipango ya kwenda kwenye sayari mbalimbali kwa lengo
la kutafuta sayari yenye kufaa kwa maisha ya binadamu.
Sisi tutaendelea kuwa na mijadala ya kutafuta fefha kwa
matundu ya choo. Hadi lini! Najua lilikuwa uamuzi Mgumu sana Mhe.
Rais na Waziri wako wa Elimu. Lakini hapakuwa na njia.
Nashukuru kama wazazi mlifanya jitihada za kuwaelekezea
vijana hao penginepo ili rasilimali watu za Taifa zisipotee na wao pia
wanufaike na rasilimali za Taifa lao. Ni haki yao.
Haikuishia tu kwenye
fedha.
Bandarini Kontainer
zaidi ya 11,000 zinaingizwa
bila kulipiwa kodi na ushuru mbalimbali. Hii ikasababisha milango na
mirija ya ukwepaji kodi kufungwa.
Na dhihiri waliokuwa wakinufaika na kupata “ super profit”
kwa kukwepa kodi wataikimbia Bandari yetu. Kitendo cha kuikimbia Bandari, kwa
muda athari yake ni kuwa bidhaa zitapungua, na makusanyo ya kodi za Serikali pia
yatapotea.
Mzunguko wa fedha katika ujumla wako nao utapungua. Na hivyo
hali ya maisha kuwa ngumu kwa kila kundi.
Ndugu zangu, kwa kiongozi yeyote jasiri, mwadilifu, mpenda
Taifa lake anakutana na mtihani mkubwa sana. Aidha ni uchaguzi mgumu. Au
aache uozo huo wote kuanzia “ hewa” hadi “
ukwepaji kodi uendelee au
audhibiti kwa njia zote
zinazowezekana.
Akiuruhusu maana yake nimkuwa mzunguko bandia wa fedha
utaendelea kuwepo na kundi dogo linalofikiwa na
mzunguko huo litaendelea kunufaika lakini umma
mpana utaendelea kuumia, kama tulivyokuwa tukiumia kabla ya uchaguzi.
Kwa bahati mbaya walio wengi ambao walikuwa hawanufaiki na
uozo uliokuwa ukiendelea hawakuwa na pa kusemea.
Leo angalau wamempata
Rais anayewasemea wao.
Rais amekuwa akitumia neno
“wapiga dili”.
Ni kweli waliokuwa wakinufaika ni hao wapiga dili
waliotengeneza “ wafanyikazi hewa, hewa, hewa, kila sekta”.
Lakini kwa bahati mbaya wanaoathirika ni
pamoja na mama lishe, na wafanyibiashara
ndogo ndogo ambao kimsingi hawahusiki kwa lolote lile na kupiga
dili.
Wao wanafanya biashara wakati hao wachache wakipiga
dili. Lakini hapa ndipo palipo na msemo, “mtego wa panya
kuwakamata wahusika na wasiohusika”. Hii ndio inayoitwa “Dilemma”.
Unachagua kipi? Uache uozo
na ufisadi/ huu mkubwa
uliofilisi nchi nzima uendelee
kwa ajili ya kuwasaidia wenye biashara ndogondogo au
funga njia, kwa muda tutaumia, rudisha nchi kwenye reli na baada ya
muda fungua milango kwa biashara halali.
Kweli kwa uamuzi huu liko kundi litaumia sana. Lakini
taifa likirudi kwenye reli, kundi hilo na wote tutanufaika. Taifa
zima litanufaika.
Nina hakika
tukiisha kurudi kwenye
mstari ajira zitatoka kwa utaratibu unaotakiwa, fedha za
miradi zitatoka na mzunguko wa fedha utarudi kama kawaida. Maamuzi
magumu yanahitaji kushirikiana lakini pia uvumilivu mkubwa. Hakuna jambo jema
linapatikana kirahisi.
Najua kuwa kuna wengi wanalalamika. Wako wasomi kati yao.
Lakini kama wasomi hao wana dhamira
njema, miaka yote nchi
ilipokuwa inatopea kwenye
dimbwi la ufisadi, uwizi huu;
mbona walikaa kimya?
Mbona hatujusikia sauti
yao. Wasomi hao wengine
wao si ndio walikuwa pia wakikusanya mamilioni wakati
mwingine kwa “Dola Za Marekani” kwa kilichokuwa kikiitwa kazi za kiushauri
yaani Consultancies?
Wengine walikuwa wakiandika rasimu za sheria mbovu lakini
wakiishia kujikusanyia mamilioni ya fedha. Kwa bahati nzuri sizungumzii nadharia.
Ninayafahamu yote ninayosema kwa undani.
Mambo ya “ Watumishi hewa”, wanafunzi hewa Kamati ya Bunge
ya Hesabu ya Serikali za Mitaa tulianza kuyazungumzia mwaka 2007.
Mbona tangu wakati huo wakati huo
hatukumwona msomi yeyote akifanyia utafiti ( hata baada ya
kuwarahisishia kwa taarifa za LAAC).
Tuache kudanganyana. Hawa wasomi wetu hawakuona
huo ufisadi , wizi na uozo huu
wakati ulipoanza ? Leo ndiyo
wanaona uchungu au kwa
sababu kwa namna moja au
nyingine na wao pia wameguswa? Japo si wasomi wote.
Watu wanalalamikia
safari za nje kuzuiwa.
Tena wanaihusisha na mgawanyo
wa mamlaka na kuwa Rais
anaingilia mamlaka zingine.
Hivi mwaka 2014 nilipotaka Bunge
kufanyiwa “Special Audit” kwa
ziara za kibunge zilizokuwa
zikitumbua fedha bila manufaa kwa taifa walikuwa wapi?
Ni sekta ipi katika nchi yetu ambayo haikuguswa na Ufisadi?
Hatimaye mwajibikaji mkuu wa fedha za Umma ni Rais kwa mujibu wa Katiba. Iweje
basi akichukua hatua ionekane kuwa ameingilia mamlaka zao?
Ni kweli siyo kila kitu cha Serikali ya Awamu ya Tano mimi
naunga mkono. Mimi siungi mkono kujenga reli kwa fedha
nyingi kwa Standard Gauge. Labda tuambiwe kuwa wakati inajengwa kwa
Standard Gauge wanazungumzia pia Electrification.
Nilikwishasema “ we do not have to re- invent the wheel”.
Leo unatoka Hamburg kwenda Munich Ujerumani takribani umbali wa kilomita 1500
kwa muda wa saa 3 tu. Sisi tunakwenda Dar- Mwanza na treni inachukua siku tatu
hadi nne.
Hii ni karne ya sayansi, hatuhitaji kuwekeza fedha kama
hatutaenda kisasa. Inatakiwa
mtu alalale nyumbani kwake
Mwanza anaenda kufanya kazi Dar na kinyume chake.
Tunataka bidhaa za viwanda na za kilimo zizalishwe kwa wingi
Mwanza, Mbeya na Kigoma na zifike katika Bandari ya Dar es Salaam kwa muda
usiozidi saa tatu na si baada ya wiki.
Nchi hii haiwezi kuendelea kwa namna ya kufikiri ya mwaka
1947. Wasomi wetu wana jukumu la kujitafakari na kubadilisha namna yao ya
kufikiri na kutoa mchango kwa taifa kama wanahitaji tuwatambue kwa usomi
wao.
Wanasiasa wetu nao ajenda isiwe kuingia Ikulu pekee. Ajenda
iwe namna ya kuliondoa taifa kwenye “ mduara” ( Vicious Circle) tulioko na
mkakati walio nao wa kulipeleka taifa tunakotaka.
Kwa ujumla nchi
ilikosa mtu wa kusimamia
rasilimali. Nchi ilikosa mtu
wa kutoa maagizo na maamuzi. Nchi
ilikosa usimamizi na
mtu wa kukemea. Rais JPM
amejidhihirisha kuwa anayo nia, anayo dhamira na anao
ujasiri na uwezo wa kufanya.
No comments:
Post a Comment