SIMBA jana ilijiweka kwenye wakati
mgumu wa kuendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Bara baada ya
kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Azam.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye
uwanja wa taifa Dar es Salaam, Simba ilihitaji ushindi au sare kuendelea
kujinafasi kileleni mwa msimamo huo lakini sasa matokeo hayo yanaifanya kutoa
nafasi kwa mtani wake wa jadi Yanga kuongoza.
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga
leo watakuwa uwanjani hapo kucheza na Mwadui na inapewa nafasi kubwa ya
kushinda kutokana na ubora wa kikosi chake kulinganisha na wapinzani wao Mwadui
ambao katika mechi ya raundi ya kwanza iliwafunga mabao 2-0 mjini Shinyanga.
Yanga ikishinda leo itafikisha pointi
46 na hivyo kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Simba yenye
pointi 45.
Muuaji wa Simba jana alikuwa John
Bocco aliyefunga bao hilo katika dakika ya 70 kwa kuuwahi mpira uliokuwa
ukimilikiwa na Method Mwanjali kabla ya kuachia shuti lililotikisa nyavu za
kipa Mghana wa Simba Daniel Agyey.
Hii ni mara ya pili kipa huyo
kufungwa na Azam tangu alipojiunga na Simba kwenye usajili wa dirisha dogo,
kipigo cha kwanza ilikuwa kwenye fainali za kombe la Mapinduzi ambapo Simba pia
ililala kwa bao 1-0 lililofungwa na Himid Mao. Mechi hiyo ilipooza karibu
kipindi chote cha kwanza ambapo kila upande ulionekana kucheza kwa tahadhari
kubwa.
Kipindi cha pili Azam walionekana
kuchangamka zaidi na hasa baada ya kupata bao hilo, ambapo Simba nao walianza
kufanya mashambulizi ya hapa na pale bila mafanikio.
Simba: Daniel Agyei, Janvier
Bokungu/Ibrahim Ajib, Mohammed Hussein, Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas
Mkude, Said Ndemla, Jamal Mnyate/Shiza Kichuya, Muzamil Yassin, Pastory Athanas
na Juma Luizio/Laudit Mavugo.
Azam FC: Aishi Manula, Erasto Nyoni,
Gardiel Michael, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Stephan Kingue/Mudathir Yahya,
Himid Mao, Joseph Mahundi, Frank Domayo, John Bocco/Abdallah Kher na Ramadhani
Singano/ Yahya Mohammed.
No comments:
Post a Comment