WAKATI imeelezwa kuwa waokoaji katika mgodi wa dhahabu wa RZ Union
ulioko Geita , wamebakiza mita tatu kuwafikia waliofukiwa Naibu Waziri
wa Nishati na Madini, Medard Kalemani akizungumza na ndugu wa watu
waliofukiwa amesema kwamba wanafanya mpango wa kuwapelekea chakula
wachimbaji hao.
Amesema kwamba jana wamefanikiwa kufanya mawasiliano na wachimbaji
hao na kwamba wapo kumi na watano na kuwa wanachohitaji kwa sasa ni
chakula.
Alisema waokoaji walifanikiwa kuwafikishia kamba na kalamu watu hao
ambao waliandika mahitaji yao na kusema kwamba wote wapo salama.
Awali akizungumza na gazeti hili akiwa eneo la tukio jana, Mkuu wa
Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga alisema kuwa bado walikuwa hawajawafikia
watu hao lakini wamefika chini sana na kukaribia njia hizo za Mlalo.
“Kinachofanyika sasa ni kuondoa udongo kwenye njia kwa kutumia watu
kwa kufanya taratibu na kwa umakini mkubwa ili udongo usiporomoke tena
katika eneo hilo,” alisema.
Alieleza kuwa matumaini yao ya kuwakuta watu hao wakiwa hai bado ni
makubwa kwani uokoaji huo unafanyika kwa umakini lakini kwa haraka sana
na sehermu iliyobaki kufikia njia hizo ni ndogo sana.
Watu hao akiwemo raia wa China mmoja walifukiwa na kifusi juzi usiku
baada ya udongo kukatika na kuziba mlango waliokuwa wakitumia kuingia na
kutoka na uokoaji unaendelea kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya
uokoaji.
Kyunga alieleza kuwa watu wengi wapo katika eneo hilo wakiwemo ndugu
wa waliofukiwa lakini kwa juhudi wanazoziona za uokoaji wametulia na
kufuata maelekezo wanayopewa ikiwemo kukaa mita 500 toka eneo la tukio.
Alisema wametakiwa kukaa mbali na eneo hilo la uokoaji ili
wasisongamane na watu wanaoendelea na uokoaji ili kuwapa fursa nzuri ya
vikosi vyote kujadiliana namna ya kufanywa kwa ajili ya kufanikisha
uokoaji huo.
No comments:
Post a Comment